Kocha wa mpito wa Chelsea, Guus Hiddink anaamini timu yake watavuka
hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) licha ya kufungwa na
Paris Saint-Germain 2-1.
Hiddink anasema kwamba bado wana fursa ‘50-50’ ya kusonga mbele,
ikizingatiwa kwamba walifungiwa ugenini na wao kupata bao moja, kwenye
mechi hiyo ya mkondo wa kwanza katika hatua ya 16 bora.
Alikuwa ni Zlatan Ibrahimovic aliyeanza kucheka na nyavu za Chelsea
kabla ya John Mikel Obi kusawazisha, lakini Edinson Cavani akawapa
wenyeji ushindi.
Mechi ya marudiano itafanyika Stamford Bridge Machi 9 na Hiddink
anasema alifurahi kwamba walifunga, japokuwa alisikitika kupoteza
mechi.
Huu ni msimu wa tatu mfululizo Chelsea wanakutana na PSG katika mechi
hizo, ambapo msimu uliopita mabingwa hao wa England walitolewa katika
hatua kama hii na PSG.
Cavani, mshambuliaji wa Uruguay aliyejiunga PSG kwa pauni milioni 55
mwaka 2013, alitokea benchi na kuwapa bao muhimu mabingwa hao wa
Ufaransa.
Chelsea wka upande mwingine kwenye benchi lao walikuwa na akina Ruben
Loftus-Cheek, Bertrand Traore, Kenedy na Matt Miazga, ndipo Hiddink
akasema aliwaonea wivu PSG kuweza kumweka benchi mtu kama Cavani.
“Niliwaonea wivu kidogo jinsi walivyokuwa na kikosi kizito uwanjani na
benchi pia. Ukiona kile timu ilicholeta kipindi cha pili – ni
wachezaji wa kimataifa hasa waliokuwa benchi. PSG ni timu kubwa sana,”
akasema Mdachi huyo.
Cavani kwa muda mwingi amekuwa akitumiwa kama papili wa Ibrahimovic au
akicheza nyuma yake, yaani namba 10.
Kwa hali hiyo amekuwa akihusishwa na kutaka kuhamia timu nyingine ili
apate muda zaidi wa kucheza, hasa kama mshambuliaji wa kati, nafasi
anayoimudu vyema.
Katika mechi nyingine ya UCL, Benfica waliwafunga Zenit St-Petersburg
1-0, kwa bao la dakika za majeruhi la kichwa la Jonas, wakicheza
nyumbani.
Mshambuliaji huyo wa Brazil aliutendea haki mpira wa adhabu ndogo wa
Nicolas Gaitan, na ni bao lake la 25 msimu huu.
Mlinzi wa wageni, Domenico Criscito alitolewa nje baada ya kupata kadi
mbili za njano kwa kucheza rafu.
Benfica walicheza vyema zaidi katika kipindi cha pili dhidi ya Zenit
ambao hawakuwa wamecheza mechi kwa wiki 10 hadi hii ya Jumanne, kwani
ligi ya kwao ipo katika mapumziko ya msimu wa baridi.