Klabu ya Chelsea imemsajili winga wa Basel ya Uswisi kutoka Misri, Mohamed Salah aliyewatesa kwenye mechi za Ligi ya Europa.
Usajili huo unadaiwa kuwa na gharama ya kadiri ya pauni milioni 11 na unakuja wakati klabu hiyo imemwachia kiungo mchezeshaji Juan Mata kwenda Manchester United kwa pauni milioni 37 hivi ambazo si kawaida Man U kuziachia kihivyo.
Salah (21) alitarajiwa kuchukuliwa vipimo kiafya hapo Stamford Bridge na pia kukutana naye kwa ajili ya makubaliano baina yao na yeye kwa mafao yake.
Hatua hii inakuja wakati Liverpool walishaanza mazungumzo na Basel kwa ajili ya kumchukua raia huyo wa Misri kwa ajili ya kumsajili kwenye dirisha dogo Januari hii.
Chelsea tayari wamemsajili Nemanja Matic. Salah aliwafunga Chelsea kwenye nusu fainali ya Europa mwaka jana kabla ya kupata bao pekee dhidi ya klabu hiyo ya kocha Jose Mourinho Desemba katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.