Matumaini ya Chelsea kutwaa ubingwa yamezidi kuyeyuka baada ya kufungwa 2-1 na Sunderland wanaoshika mkia wa Ligi Kuu ya England (EPL).
matokeo hayo yamewapa nafasi kubwa Liverpool kuchukua ubingwa, na watajilaumu wenyewe ikiwa wataukosa ubingwa huo kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 24.
Chelsea walianza vyema mechi hiyo kwa Samuel Eto’o kupachika bao dakika ya 12 lakini likasawazishwa na Connor Wickham na Fabio Borini aliyetoka Liverpool kufunga kwa penati baada ya Cesar Azpilicueta kumchezea rafu Jozy Altidore.
Hii ni mechi ya kwanza kwa Jose Mourinho kupoteza katika uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge katika mechi 78 alizosimamia. Kocha msaidizi wa Chelsea, Rui Faria alitaka kumvaa mwamuzi Mike Dean lakini Mourinho akamzuia.
Chelsea hawakutarajia matokeo kama hayo yaliyowaacha pointi mbili nyuma ya vinara Liverpool ambao wanacheza dhidi ya Norwich Jumapili hii na wiki ijayo watakipiga na Chelsea.
Sunderland wamekuwa kikwazo kwa timu zinazosaka ubingwa, kwani mechi iliyopita walitoa sare na Manchester City wanaoshika nafasi ya tatu na wamekuwa msaada mkubwa kwa Liverpool.
Chelsea wanatakiwa kujipanga upya, kwani kabla ya kukabiliana na Liverpool, watacheza na Atletico Madrid ugenini Jumanne hii.
Kama alivyozoea, Mourinho aliwalaumu washambuliaji wake, akisema kwamba kuna kitu wanakosa na kwamba walikuwa na nafasi 31 za kufunga lakini wakafanya hovyo.
Mfungaji anayeongoza Chelsea kwa sasa ni kiungo Eden Hazard ambaye ni majeruhi.
Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspur waliwafunga Fulham 3-1 na kuwaongezea wapinzani hao wa London nafasi ya kushuka daraja msimu huu.
Aston Villa walitoshana nguvu kwa suluhu na Southampton, Cardiff wakaenda sare ya 1-1 na Stoke, Newcastle wakalala nyumbani kwa mabao 1-2 dhidi ya Swansea wakati West Ham nao walipigwa 1-0.
Jumapili hii Hull wanawakaribisha Arsenal wanaoshika nafasi ya nne huku Everton walio nafasi ya tano wakiwakaribisha Manchester United na kocha wao wa zamani, David Moyes.