*Southampton na Man City wamekaa vizuri
*Man United, Liverpool bado hawapo vyema
Mzunguko wa sita wa Ligi Kuu England umewaacha Chelsea wakifurahia kileleni, baada ya kuwa na matokeo ya ushindi katika mechi tano na sare ya mechi moja.
Mshambuliaji wao mpya kutoka Atletico Madrid, Diego Costa ameendeleza makali yake kwa kufunga katika kila mechi, licha ya kwamba anasumbuliwa na maumivu.
Vijana wa Jose Mourinho wamejikusanyia pointi 16 kati ya 18 ambazo wangeweza kujikusanyia, kama si kwenda sare na Manchester City kwenye mchezo pekee ambao hawakushinda. Costa mwenyewe amefunga mabao manane, huku kocha wake akisema mara nyingi hafanyi mazoezi.
Southampton waliotarajiwa kufanya vibaya sana msimu huu kutokana na wachezaji wake bora zaidi watano kuporwa na klabu kubwa, wanashika nafasi ya pili.
Saints walio chini ya kocha Ronald Koeman wamefikisha pointi 13, wakiwa mbele ya mabingwa watetezi, Manchester City wenye pointi 11.
City wanaonolewa na Manuel Pellegrini wameshapokea kichapo mara moja na wana mtihani mkubwa kuchuana na Chelsea.
Arsenal wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 10 sawa na Swansea na Aston Villa. Washika Bunduki wa London wamshinda mechi mbili na kwenda sare nne, hali inayomfadhaisha Arsene Wenger.
Manchester United ambao bado hawajaamka licha ya kuwa na sura nyingi mpya za wachezaji wazuri, ambapo wanashika nafasi ya saba, ile ile waliyomalizia msimu uliopita na kukosa mechi za kimataifa msimu huu.
Kocha Louis van Gaal bado anajiuliza kipi cha kufanya kwenye kikosi kilichojaa nyota, hasa maeneo ya ushambuliaji, na wikiendi hii nahodha wao, Wayne Rooney alitolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, hivyo atakosa mechi tatu muhimu, ikiwamo dhidi ya Chelsea.
Mashetani Wekundu wanafungana pointi na Tottenham Hotspur, Crystal Palace na Leicester – wote wakiwa na pointi nane.
West Ham waliowaadhiri Liverpool kwa kuwafunga wanashika nafasi ya 11 huku Liver wenyewe wakisuasua katika nafasi ya 12 tofauti kabisa na msimu uliopita walipokaribia kutwaa ubingwa. Liverpool wanawakosa wafungaji wao wa msimu uliopita, Luis Suarez aliyehamia Barcelona na Daniel Sturridge aliyeumia. Timu zote zina pointi saba.
Everton wanashika nafasi ya 13 wakifungana pointi sita na Hull wakati Sunderland wako pointi tano sawa na Stoke na West Bromwich Albion, wote watatu wakiwa umbali wa pointi moja tu kutumbukia kwenye eneo la hatari la timu tatu zinazoshika mkia.
Wengine walio nafasi mbaya hadi sasa ni Queen Park Rangers (QPR), Burnley na Newcastle ambao kocha wao, Alan Pardew anatakiwa kufukuzwa na washabiki wao.