Timu za England zimeendelea kupepesuka kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Chelsea walibanwa nyumbani Stamford Bridge kwa kwenda sare ya 1-1 na Schalke ya Ujerumani wakati huko Ujerumani Manchester City wamedungwa 1-0 na Bayern Munich.
Mbali na kushindwa kupata ushindi uliotarajiwa, Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho anasema ana wasiwasi kuwa mshambuliaji wake tegemeo, Diego Costa hayupo timamu kimwili kucheza mechi nyingi.
Mourinho anasema kwamba mchezaji huyo aliyemnunua kwa pauni milioni 34 kutoka Atletico Madrid hawezi kucheza zaidi ya mechi moja kwa wiki, na Jumatano hii aliiingia dakika ya 74.
Aliumia nyama za paja Septemba 4 alipokuwa akichezea taifa lake la Hispania lakini kabla ya hapo amekuwa majeruhi, hasa kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita.
Mourinho anasema kwamba Costa anahitaji wiki moja kwa ajili ya kuruhusu misuli yake kurejea katika hali ya kawaida na Mourinho amesikitishwa na kukosa ushindi kwenye mechi yao ya kwanza UCL.
Chelsea walipata bao dakika ya 11 kupitia kwa kiungo Cesc Fabregas huku Didier Drogba akishindwa kuwa hai na hatari mchezoni, na dakika ya 60 Klaas-Jan Huntelaar alifunga bao la kusawazisha.
Chelsea waliovuna pointi zote 12 katika mechi nne, wanasafiri kucheza na Manchester City Jumapili hii.
Mourinho anasema siku tatu hazingemtosha Costa kurudia hali ya utimamua wa mwili na wala si kwamba hakumwanzisha ili kumsubirishia mechi ya Jumapili.
Drogba alicheza kwa mara ya kwanza kwa Chelsea katika UCL tangu alipofunga penati ya mwisho na kuwapa ubingwa wa Ulaya 2012 lakini alishindwa kufunga bao baada ya kutiliwa mpira vizuri na Eden Hazard.
MANCHESTER CITY WAPIGWA UJERUMANI
Manchester City wameshindwa kurudia walichofanya msimu uliopita walipowafunga Bayern Munich, kwani Jerome Boateng aliwafungia mabingwa hao wa Ujerumani bao katika dakika ya 90.
Baada ya kipa wa Man City, Joe Hart kuwa imara golini akionesha ushujaa wake, alisalimu amri dakika ya 90 na mbaya zaidi Sergio Aguero akakosa nafasi dhahiri ya kusawazisha dakika za lala salama.
Boating ni beki wa zamani wa City na shuti lake kali lilimparaza kidogo Mario Gotze na kumvuka Hart ambaye hakuamini baada ya City kushindwa kufagia mpira wa kona.
Mwingereza Hart alifanikiwa awali kuwabakiza City mchezoni kwa kuokoa mipira iliyokuwa ikiingia golini ya Thomas Muller, Gotze na Boateng.
City walilalamika kwa kutopewa penati pale Mehdi Benatia alipoonekana kama vile amemchezea vibaya David Silva ndani ya eneo la penati.
Wapinzani wao kwenye Kundi E, Roma ya Italia walianza kishari kwa kuwachakaza CSKA Moscow ya Urusi 5-1.
Man Cty wapo katika shinikizo la kuvuka hatua za makundi, kwani mmiliki wao, Sheikh Mansour anataka wafike mbali na hata watwae kombe hilo, akiamini wanastaghili heshima hiyo.
Kiungo Yaya Toure alishindwa kung’ara kwenye mechi hiyo akiwa kana kwamba hakuwa fiti na Bayern ndio walitawala eneo la kiungo.