*Jose Mourinho, Ramires, Willian kadi nyekundu
*Man City pungufu, Southampton, Stoke wapeta
*Everton waamka, Stoke, Albion na Fulham safi
*”Advantage Man City”
Chelsea wamepata pigo katika mbio zao za ubingwa baada ya kufungwa 1-0 na Aston Villa kwenye mechi ambayo kocha wao na wachezaji wawili walilimwa kadi nyekundu.
Chelsea walisherehekea kile walichodhani ni bao mwishoni mwa nusu ya kwanza ya mchezo, lakini ikabainika kwamba mfungaji, Nemanja Manic alikuwa ameshika mpira kabla ya kuutia kimiani kutokana na kona.
Badala yake, furaha ilikuwa kwa wenyeji Villa waliopata bao kupitia kwa Fabian Delph aliyenasa majalo ya Marc Albrighton muda mfupi baada ya Willian kupewa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa nyekundu.
Lakini pia Mbrazili Ramires na kocha Jose Mourinho waliagizwa kutoka nje na mwamuzi baada ya kuonesha hasira kali karibu na mwisho wa mchezo.
Ramires alifanya rafu mbaya ya miguu miwili dhidi ya Karim El Ahmadi na alipotolewa nje Mourinho aliwaka kumpinga mwamuzi, naye akatolewa nje.
Hata hivyo, Chelsea wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 66, zikiwa ni sita mbele ya wanaowafuatia, Manchester City ambao hata hivyo wana mechi tatu pungufu ya Chelsea.
MAN CITY PUNGUFU WAWAZIDI NGUVU HULL
Manchester City walifanikiwa kupata ushindi dhidi ya timu inayoelekea kuimarika ya Hull City, licha ya kuwa pungufu kwa mtu mmoja kutokana na nahodha wake, Vincent Kompany kutolewa nje kwa kadi nyekundu ndani ya dakika 10 za kipindi cha kwanza.
City walipata bao la kuongoza muda mfupi tu baada ya kupunguzwa mtu, kwa bao alilofunga David Silva. Kompany alitolewa nje kwa rafu dhidi ya Nikica Jelavic. Company alifadhaishwa kwa kadi hiyo kiasi cha kupigiza ukuta kwa mguu wakati akitoka nje, kwani inadaiwa Jelavic alimchezea rafu kwanza kabla ya yeye kujibu.
City waliwamudu Hull ambao Jumamosi hii hawakuonesha machachari makubwa, kwani dakika za mwisho Edin Dzeko alifunga bao la pili, akipigilia msumari kwenye jeneza la Hull.
Hull kwa kupoteza mechi hiyo sasa wanashika nafasi ya 13 wakiwa na pointi 30, nafasi ambayo si nzuri sana kwani timu zilizo nafasi ya kushuka daraja zina pointi 24 na nyingine 25.
EVERTON WAPAMBANA KULINDA HESHIMA
Katika mechi nyingine iliyokuwa na ushindani mkubwa katika dimba la Everton la Goodison Park, wenyeji walifanikiwa kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Cardiff.
Hata hivyo, ilibidi Toffees wasubiri hadi dakika ya 90 kupata bao la ushindi, kwani walikuwa sare kutokana na mabao ya Deulofeu katika dakika ya 59 lililosawazishwa na Torres Ruiz dakika ya 68 kabla ya Seamus Coleman kuachia mkwaju uliojaa wavuni kwenye piga nikupige na kuwapa ushindi muhimu Everton.
Kwa ushindi huo, Everton wanaofundishwa na Roberto Martinez wanashika nafasi ya sita, ikiwa ni moja mbele ya Manchester United waliorudishwa nyuma nafasi moja na wana michezo sawa, japokuwa United wanacheza tena Jumapili hii.
Everton wana pointi 51, nyuma ya Tottenham Hotspur waliofikisha pointi 53 lakini wana mchezo mmoja zaidi ya Everton na Man U, juu yao wakiwapo Arsenal na Liverpool wenye pointi 59.
MATOKEO MENGINE YA EPL
Katika mechi nyingine za Jumamosi hii, Fulham waliwaduwaza Newcastle kwa kuwapiga bao 1-0 na kuweka hai matumaini ya kocha Pepe Mel kubaki Craven Cottage hapa London.
Southampton waliwatoa ushamba Norwich kwa kuwakandika bao 4-2, Stoke wakawaadhibu West Ham 3-1, Swansea wakapoteza mechi kwa 1-2 dhidi ya West Bromwich Albion huku Sunderland wakienda suluhu na Crystal Palace.
Mkiani kabisa mwa ligi bado ni Fulham wenye pointi 24, Cardiff 25 sawa na Sunderland lakini Sunderland wana mechi tatu kuliko timu mbili hizo.
Palace wana pointi 28 sawa na West Brom huku Norwich na Swansea wakiwa na pointi 29 kila moja wakizidiwa na Hull wenye 30 na West Ham waliojikusanyia 31.
Stoke wamejiweka pazuri kwa kufikisha pointi 34 katika nafasi ya 11 sawa na Villa.
Jumapili hii mtoto hatumwi dukani kwani mahasimu wakubwa na watani wa jadi wa soka la England, Liverpool na Manchester United wanakwaana huku London Kaskazini ikiwaka moto kwa mechi baina ya mahasimu Arsenal na Tottenham Hotspur.