Septemba 12 mwaka huu msimu mpya wa Ligi kuu England. Maandalizi ya msimu tayari yameanza kwa timu mbalimbali. Wageni wa Ligi hiyo Leeds United nao wamefanya usajili kuimarisha kikosi chao kwa kumchukua mshambuliaji hodari wa Valencia, Rodrigo. Lakini gumzo kubwa lipo kwa kikosi cha Frank Lampard yaani Chelsea.
Timu hiyo ilitumikia adhabu ya kutofanya usajili hivyo imetumia kipindi hiki kusajili wachezaji kadhaa kwa mkupuo. Swali moja linaloulizwa kwa sasa; ni namna Chelsea wapo tayari kupigania ubingwa? Frank Lampard ana kikosi cha kwanza na akiba chenye thamani ya pauni milioni 250.
Chelsea si kama timu zingine, wao hawakutumiafedha msimu uliopita kufanya usajili kwa sababu walifungiwa, lakini timu nyingi kwa sasa zinakabiliwa na ukata kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Wahenga wanasema mtu anapokosekana ndipo pengo lake linajulikana kuwa lipo ama halipo. Chelsea kutofanya usajili msimu uliopita kumewapa somo mujarabu na sasa wamefanya usajili wao haraka haraka ili kujipanga kwa msimu ujao. Je, nani na nani watakuwa kwenye kikosi cha Frank Lampard?
THIAGO SILVA
Thiago Silva ni jina kubwa katika kandanda. Ni beki mahiri ambaye amecheza Ligi Kuu mbili muhimu kwa mchezaji; Ligi Kuu Italia na Ufaransa, hiyo ni pamoja na Ligi Kuu Brazil. Silva alikuwa na wakati bora kabisa katika kikosi cha AC Milan kabla ya kuuzwa kwenda vigogo wa soka nchini Ufaransa, PSG. Chelsea wamemsajili Thiago Silva kama mchezaji huru ambaye alishamaliza mkataba wake na PSG.
HAKIM ZIYECH
Huyu alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Frank Lampard kutoka klabu ya Ajax Amsterdam kwa kiasi cha pauni milioni 38. Ziyech alikuwa kwenye kikosi cha Ajax kilichojaa chipukizi wengi ambao walifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Ziyech ni raia wa Morocco na Uholanzi. Ni winga na kiungo mahiri, mzuri kiufundi na binafsi akifananishwa na uwezo wa Riyad Mahrez wa Manchester City.
TIMO WERNER
Ghadhabu za Chelsea katika usajili zimemkumba mshambuliaji wa Werder Bremen, Timo Werner. Chelsea waliwazidi ujanja mabingwa wa England, Liverpool kwa kulipa pauni milioni 53 ili kupata huduma ya Timo Werner.ni mshambuliaji ambaye amekuwa akipachika mabao maridadi, akitarajiwa kuimarisha safu ya ushambuliaji wa Chelsea ambayo imekuwa ikiwategemea chipukizi Tammy Abraham na mkongwe Oliver Giroud. Werner alipachika mabao 34 msimu uliopita.
KAI HAVERTZ
Bayer Leverkusen hawakuwa na hiana wakati ofa ya pauni milioni 90 ilipowasilishwa mezani kwao. Hawakutumia muda mwingi kutafakari zaidi ya kukubali kuwa kipaji cha Kai Havertz kilistahili kulipiwa kiasi hicho. Kai kama ilivyo kwa Timo Werner wameonesha vipaji vyao katika Ligi Kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga. Ni mchezaji mwenye ari na umri sahihi kuitumia Chelsea.
BEN CHILWELL
Nafasi ya Marco Alonso na Emmerson imepata mshindani mwingine. Ni Ben Chilwell kutoka kwa mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu England, Leicester City. Mabosi wa Licester City hawakuona sababu ya kukataa ofa ya pauni milioni 50 ili kumruhusu beki huyo wa kushoto kutua katika kikosi cha Chelsea.
MALANG SARR
Kama ilivyo kwa Thiago Silva kujiunga Chelsea kama mchezaji huru ndivyo ilivyo kwa Malang Sarr. Hata hivyo Chelsea wamepanga kumtoa kwa mkopo Malang Sarr ili kuongeza uzoefu wake zaidi.
Chelsea waliruhusu mabao 79 katika mashindano yote msimu uliopita. Msimu ujao wanaonekana kuchanganya wachezaji chipukizi na wakongwe.
ANDRE ONANA?
Bado Chelsea hawajamsajili Andre Onana mlinda mlango kutoka Ajax Masterdam, lakini jina lake linatajwa kuwa miongoni mwa makipa wanaohitajika Stamford Bridge. Lampard anahitaji golikipa wa kuziba pengo la Kepa Arrizabalga, na huenda wakampata Onana kwa gharama ya pauni milioni 30. Kepa analaumiwa kwa kufanya makosa mengi msimu uliopita na kuigharimu timu katika mechi mbalimbali.
Karatasi ya Frank Lampard inaonesha kikosi cjake kipo tayari kupigania ubingwa msimu ujao na lazima suala hilo liwe kipaumbele. Usajili unaofanywa sasa ni kuboresha kikosi cha kutoa wigo mpana ambao utamwezesha kuchagua wachezaji wa kupangwa mechi 38 za Ligi Kuu na Ligi Mabingwa Ulaya.
Kikosi hicho kinaonesha Lampard anahitaji wachezaji wenye malengo makubwa na viwango vya juu. Changamoto pekee ambayo inaweza kumrudisha nyuma ni iwapo kuna wachezaji wake wapya watagundulika kuambikizwa ugonjwa wa Corona. Wachezaji wake waliopo ambao waligundulika kuambikizwa corona na wakajiweka karantini ni Mason Mount, Tammy Abraham, Christian Pulisic na Fikayo Tomori, pamoja na Ross Barkley, Michy Batshuayi, Jorginho na Emerson.
Lampard anaweza kuchukizwa na hali hiyo kwa kiasi fulani kwani itakuwa inarudisha nyuma malengo yake. hata hivyo inaonekana amepanga kuwatumia Mason Mount na Pulisic, huku akiwa na matumiani ya kutumia Kai Havertz kucheza nyuma ya mshambuliaji Timo Werner
Havertz amewindwa kwa muda mrefu na Lampard kwa vile imepangwa itengenezwe kombinesheni na Pulisic na Mount kuwatetemesha mabeki wa timu pinzani.
Hata hivyo Mount na Pulisic wnatarajiwa kukosa mechi za mwanzo wa msimu huu kutokana na kutakiwa kukaa karantini kwa siku 10 lakini Lampard anaweza kumtumia Hakim Ziyech kuwa mbadala wao.
Ziyech amejaliwa kipaji kikubwa, lakini kuwa na Kai Havertz kikosini itamuwia vigumu Lampard kuchagua mchezaji wa kuanza kikosi cha kwanza. ZIyech na Kai si busara kuwapanga katika kikosi cha kwanza pamoja, badala yake Lampard atatakiwa kuchagua mmoja wa kuanza mechi. Katika eneo la kiungo Lampard atakuwa na wachezaji wawili muhimu N’golo Kante na Mateo Mateo Kovacic ambaye alicgauliwa kuwa mchezaji bora wa msimu wa Chelsea.
Lampard ameshindwa kumwendeleza beki chipukizi wa kushoto, Emmerson na hajaridhishwa na kiwango cha Marcos Alonso ndio maana amemsajili Ben Chilwell ambaye anatarajiwa kuwa chaguo la kwanza kwa sababu ana uwezo wa kulinda lango na kushambulia kupitia pembeni.
Kurt Zouma amecheza vizuri msimu uliopita, lakini hajafikia matakwa ya benchi la ufundi. Hivyo kuwasili kwa Thiago Silva kunampa nafasi ya kujifunza na kuwa mchezaji muhimu zaidi kikosini. Silva anatarajiwa kutoa mchango mkubwa kuboresha kiwango cha Zouma.
Aidha, huenda Thiago Silva akawa nahodha mpya wa Chelsea kuwaongoza vijana kama Tammy Abraham, Ross Barkley, Callum Hudson-Odoi, Billy Gilmour, Ruben Loftus-Cheek na Tomori, pamoja na wengine wenye uzoefu kama vile Antonio Rudiger, Cesar Azpilicueta, Olivier Giroud. Majibu ya swali letu yatapatikana mwezi Mei mwaka 2021, lakini ifikapo desemba mwaka 2020 tutaona mwanga au giza kwa Chelsea.