Bao la kusawazisha la dakika ya 80 la mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Gylfi Sigurdsson limewaacha Chelsea na Tottenham Hotspurs kwenye vita ya kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pamoja nao katika mchuano huo ni Arsenal wanaoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, wakiwa pointi mbili nyuma ya Chelsea na moja mbele ya Spurs.
Sare ya Jumatano hii inawaachia Spurs matumaini kidogo ya kufuzu mwaka huu, baada ya mwaka jana kukosa kwenye tundu la sindano, baada ya nafasi yao kuchukuliwa na Chelsea waliotwaa kombe la Ulaya, hivyo kufuzu moja kwa moja na Spurs kutupwa Ligi ya Europa.
Chelsea walitangulia kufunga kupitia kwa Oscar katika mechi iliyopigwa Stamford Bridge ambayo kocha Rafa Benitez alimkaribisha vyema Andre Villas-Boas aliyekuwa akirejea dimba alilofukuzwa kazi na Roman Abramovich.
Hata hivyo, Spurs waliotumia mamilioni ya pauni kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya kufuzu Ulaya, walisawazisha kupitia Emmanuel Adebayor dakika ya 26, lakini dakika 10 tu baadaye, Mbrazili Ramires aliwanyanyua viti washabiki wa Chelsea kwa bao lililodhaniwa lingekuwa la ushindi.
Manchester United wameshatwaa ubingwa na kufuzu Ulaya, na Manchester City pia wamefuzu kwa mashindano ya Ulaya, hivyo zimebaki nafasi mbili, ambapo ikiwa Chelsea, Arsenal na Spurs watakuwa na matokeo ya kufanana kwenye mechi zao mbili mbili zilizobaki, Spurs watatupwa nje.
Chelsea wana mechi dhidi ya Aston Villa Jumamosi hii, ambapo wakishinda watajihakikishia nafasi, wakati Spurs wana mechi nyumbani kwa Stoke City Jumapili, lakini ushindi bado hautawahakikishia chochote, maana Arsenal watacheza na Wigan Jumanne.
Mechi za mwisho Mei 19 zitashuhudia Chelsea wakiumana na Everton Stamford Bridge; Spurs wakiparurana na Sunderland ya Paolo Di Canio wakati Arsenal wakikaribishwa kaskazini mashariki mwa England na Newcastle wanaoonesha uchovu wa aina yake msimu huu, wakitishiwa pia kushuka daraja.