*Man City wavutwa shati EPL
Chelsea wameendelea kupata mapigo, baada ya kutupwa nje ya michuano ya
Kombe la FA na Everton.
Alikuwa Romelu Lukaku, mchezaji wao wa zamani ambaye hakupendwa na
bosi aliyefukuzwa kazi, Jose Mourinho aliyewapa maangamizi.
Katika mchezo huo, mshambuliaji wa Chelsea ambaye amehusishwa na
matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu, Diego Costa, anadhaniwa kumng’ata
mchezaji wa Everton, Gareth Barry na wote kuishia kupewa kadi
nyekundu, lakini kwa matukio tofauti.
Makocha wao, Guus Hiddink na Roberto Martinez hawakutoa kauli ya
kumshutumu yeyote. Mabao ya Everton yalifungwa na Lukaku na Barry
Pengine Chelsea watajilaumu kwa kumwacha Lukaku aondoke, ambapo akiwa
na umri wa miaka 22 tu ameshafunga mabao 25 katika mashindano yote
msimu huu.
Katika Ligi Kuu ya England, Manchester City walibanwa na Norwich kwa
kwenda suluhu wakati Bournemouth wakiwapiga Swansea 3-2 na Stoke
wakiwa nyumbani wakilala kwa 1-0 dhidi ya Southampton.
Hali hiyo inawaacha vinara Leicester kuwa juu kwa pointi 60, Tottenham
Hotspur wa pili kwa pointi 55, Arsenal wa tatu na zao 52 wakati Man
City wanazo 51.
Mkiani wamo Aston Villa na pointi 16 wakiwa chini ya Newcaste wenye
pointi 24 na Norwich wenye pointi 25.