Chelsea wameendelea na majanga ya kufungwa mfululizo kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kukung’utwa na Leicester 2-1.
Itabidi sasa Jose Mourinho afanye kazi ya ziada kuokoa vijana wake, vinginevyo mmiliki na bodi ya klabu wafikirie kupata mbadala wake.
Bila shaka kichapo hicho kitajenga picha mpya Stamford Bridge na huenda ukaelekea kuwa mwanzo wa mwisho wa Mreno huyo hapo. Mabao ya washindi yalifungwa na nyota wao wawili – Jamie Vardy na Riyad Mahrez huku la kufutia machozi la Chelsea likifungwa na Loic Remy.
Kocha wa Leicester ambao sasa wamerejea kileleni mwa msimamo wa ligi, Claudio Ranieri alijawa furaha, akisema kwamba wachezaji wake hao wawili hawana bei, kwa maana kwamba hawauziki kwa kitita chochote kile.
Ranieri amekuwa shujaa klabuni hapo tangu alipojiunga nao msimu wa kiangazi na kuwaondoa kwenye maeneo ya chini ya jedwali hadi kuongoza ligi nyakati tofauti, jambo ambalo halijapata kutokea katika historia ya timu hiyo.
Majuzi, kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, alisema kwamba huenda Leicester wakatwaa ubingwa msimu huu, maneno yaliyopata pia kusemwa na kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ambaye timu yake wanashika nafasi ya pili.
Chelsea wamepoteza mechi tisa kati ya 16 walizocheza, ikiwa ni rekodi mpya na mbaya zaidi kwa Mouriunho katika awamu zake mbili katika klabu hiyo ya jijini London na ni wazi kwamba sasa itakuwa ngumu kutetea ubingwa wao.
Mourinho alinukuliwa wiki iliyopita akisema kwamba si ajabu wakashindwa hata kushika anfasi nne za juu hivyo kukosa ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mourinho alieleza kwamba alihisi kuwapo dalili za usaliti.
Hata hivyo, kwenye mashindano hayo Chelsea walimaliza wakiwa vinara wa kundi lao na sasa wanaenda kwenye hatua za mtoano.
Huenda mmiliki wa klabu hiyo, bilionea Mrusi, Roman Abramovich akasubiri kuona watakavyofanya kwenye mashindano hayo ya kimataifa kabla ya kuchukua hatua, japokuwa tayari kiti hicho cha Mourinho kinaonekana kuwa cha moto