*Man U, Liverpool washinda
Vinara wa Ligi Kuu ya England, Chelsea wamepata karamu ya mabao baada ya kuwatandika Swansea 5-0.
Oscar na Diego Costa walifunga mabao mawili kila mmoja kipindi cha kwanza na kuwafanya waongoze kwa mabao manne, na katika kipindi cha pili Andre Schurrle alifunga bao la tano, hivyo kufungua pengo la pointi tano dhidi ya wanaowafuatia kwenye msimamo wa ligi.
Hiki ni kipigo kizito zaidi kwa Swansea msimu huu na mbaya zaidi kimetokea nyumbani kwao, dalili zikiwa mbaya mapema kabisa, kwani bao la kwanza lilifungwa na Oscar dakika ya kwanz atu ya mchezo. Swansea hawajashinda katika mechi nne mfululizo za ligi hiyo sasa.
Kadhalika hii ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Swansea tangu wamuuze mshambuliaji na mfungaji wao bora, Wilfried Bony kwa Manchester City. Ilikuwa wiki ngumu kwa Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho anayekabiliwa na mashitaka kutoka kwa Chama cha Soka (FA), akidaiwa kuvunja kanuni kwa kusema kuna kampeni kati ya waamuzi, vyombo vya habari na klabu nyingine dhidi ya Chelsea.
Katika mechi nyingine, Manchester United wakicheza ugenini waliwafunga Queen Park Rangers (QPR) 2-0, katika mechi ambayo kipindi cha kwanza Man U hawakucheza vyema na baadhi ya washabiki kulalamika huku wakiimba “4-4-2, shambulia, shambulia, shambulia!”
Mabao ya United yalipatikana katika kipindi cha pili, kupitia kwa mchezaji aliyetokea benchi, Marouane Fellaini katika dakika ya 58 na la pili katika dakika ya mwisho lililofungwa na James Wilson.
Katika mechi nyingine, Aston Villa walilala nyumbani walipofungwa mabao 2-0 na Liverpool, huku kocha wa Liver, Brendan Rodgers akidai kwamba vijana wake wamerudia hali njema. Mabao yao yalifungwa na Fabio Borini na Rickie Lambert.
Tottenham Hotspur walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Sunderland, Newcastle wakaloa kwa kufungwa 2-1 kna Southampton, Burnley wakafungwa 3-2 na Crystal Palace na Leicester wakapigwa 1-0 na Stoke.