*Everton waloa kwa Crystal Palace
Mahasimu wawili wa karibuni, Jose Mourinho na Manuel Pellegrini wameshindwa kutambiana katika mechi iliyoshuhudia Frank Lampard akiifunga timu yake ya zamani.
Chelsea walitangulia kupata bao kutoka kwa Andre Schurrle dakika ya 71 kabla ya Lampard kusawazisha dakika ya 85 akitokea benchi, na hakushangilia bao kwa sababu ametumikia Chelsea na kuwafungia mabao 211 katika mechi 648.
Pellegrini ambaye timu yake ilimaliza mechi wakiwa watu 10 kutokana na Pablo Zabaleta kupewa kadi nyekundu, alisema aliudhika na jinsi Chelsea aliowaita ni timu ndogo ilivyocheza kwa kuweka watu wengi kwenye ulinzi.
Alisema ni sawa na Stoke walivyofanya na kuwafunga 1-0 dimbani Etihad msimu huu akisema Jumapili hii walicheza dhidi ya timu ndogo ambayo muda wote ilikuwa ikijilinda isifungwe badala ya kucheza soka ya kueleweka.
“Nisingependa kucheza namna hiyo, wachezaji 10 wanajilinda tu kwenye eneo lao la nusu uwanja, walifunga bao kwa bahati katika shambulizi la kushitukiza na kisha wakarudi kujihami mpaka mwisho,” anasema Pellegrini.
Hiyo ilikuwa mechi ya 200 kwa kipa Joe Hart ambaye amesema hajui hatima yake katika klabu hiyo, na sasa Pellegrini amesajili kipa mwingine wa kimataifa, Willy Caballero wa Argentina.
Zabaleta alitolewa nje baada ya kuhusika katika pilika mbaya na Didier Drogba aliyeingia dakika ya 86 badala ya Diego Costa. Mourinho alimjibu mpinzani wake Pellegrini kwa kueleza kwamba mara nyingi raia huyo wa Chile hudai kwamba hataki kuzungumza kumhusu yeye au timu yake lakini anaendelea kufanya hivyo, akakataa kuzungumzia maneno yake.
EVERTON WAFUNGWA NA PALACE
Everton wameadhirika nyumbani Goodison Park baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Crystal Palace wanaofundishwa na mwalimu mpa, Neil Warnock.
Ulikuwa ushindi wa kwanza msimu huu kwa Palace na sasa Everton wa Roberto Martinez hawajashinda mechi nne zote za nyumbani. Romelu Lukaku alianza kufunga bao lililosawazishwa na Mile Jedinak kabla ya Fraizer Campbell na Yannick Bolasie kuweka wageni mbele kwa mabao yao. Leighton alifunga bao la penati ndani ya dakika 10 za mwisho lakini Palace hawakubabaika, wakabaki imara.
Everton hawakutarajiwa kufungwa, ikizingatiwa walivyocheza vyema na kuwachakaza Wolfsburg katika mechi ya Ligi ya Europa Alhamisi hii. Toffees walichezesha watu kama Christian Atsu aliye kwa mkopo kutoka Chelsea na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Samuel Eto’o na mkongwe Leon Osman lakini hawakufurukuta mbele ya ngome imara na kipa Julian Speroni.