Chelsea na Liverpool wamepangwa kuchuana kwenye nusu fainali ya Kombe la Ligi, maarufu zaidi kaa Capital One Cup.
Chelsea wanaoongoza Ligi Kuu ya England wamepata nafasi hiyo baada ya kuwachakaza Derby 3-1 wakati Liverpool waliwafunga Bornemouth 3-1 usiku wa Jumatano hii, mabao mawili yakifungwa na Raheem Sterling aliyekuwa na ukame wa mabao wa muda mrefu. Jingine lilifungwa na Lazar Markovic.
Katika nusu fainali nyingine ya kombe hili dogo, Tottenham watacheza na Sheffield United, baada ya vijana hao wa Mauricio Pochetino kufanikiwa kuwafunga Newcastle 4-0 na kuwaongezea uchungu, kwani kwenye mechi ya ligi kuu iliyopita, Arsenal waliwachakaza kwa 4-1.
Sheffield United si wa kuchezea, kwani kwenye michuano kama hii walipata kuwafunga na kuwatupa nje Southampton na West Ham. Zitakuwa mechi mbili kwa kila timu na zitachezwa mwezi ujao, huku fainali ikiwa Machi mosi mwakani.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers amefurahia matokeo hayo, ikizingatiwa kwamba hawafanyi vyema kwenye ligi kuu na amesema kwamba atajitahidi walau akapate kikombe hicho kama faraja, kwani pia wametupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ni majuzi tu walifungwa 3-0 na Manchester United kwenye ligi kuu ya England na wanakabiliana na Arsenal wikiendi hii katika michuano hiyo hiyo. Amekuwa kwenye shinikizo la timu kufanya vyema, na inadaiwa Wamarekani wanaoimiliki Liverpool wanafikiria kumfukuza iwapo timu itaendelea kufanya vibaya.