*Arsenal waanza kazi
Manchester City wamewashushia Chelsea kipigo cha mbwa mwizi katika mechi ya kwanza baina yao kwenye msimu wa Ligi Kuu ya England.
City walioanza kwa tabu mechi hiyo ya Jumapili jioni walibadilika na kuwa
wazuri kiasi cha kuwaadhibu jinsi hiyo, 3-0, mabingwa watetezi hao.
Chelsea walioanza ligi kwa kutoshana nguvu na Swansea, hawajaonesha jitihada kubwa tangu kwenyea mechi zao ziara kabla ya msimu. Jumapili hii ilikuwa ngumu kwao, ambapo licha ya kipa Asmir Begovic kuokoa hatari nyingi hatimaye walilala.
Mabao yalitiwa kimiani na Sergio Aguero mara tu baada ya nusu saa kukatika, na katika kipindi cha pili ambacho Chelsea walijitahidi kuchea vyema, nahodha Vincent Kompany alitia la pili dakika ya 79 kabla ya kiungo aliyewavuruga kabisa Chelsea, Fernandinho kutia la tatu dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho.
Kocha Jose Mourinho wa Chelsea alidai ushindi huo wa Manuel Pellegrini na City wake ni wa bandia, katika hali ya kushangaza, kwani walishindwa kwa mabao mengi. Alidai hawezi kuamini kwamba katika kipindi cha kwanza walipocheza vibaya walifungwa bao moja lakini kipindi cha pili walipokuwa vyema wakafungwa mawili.
Pellegrini kwa upande wake alidai ni kawaida ya City kuwa na ufanisi na kuwatawala Chelsea. Katika mechi mbili za ufunguzi Chelsea wameambulia pointi moja, kufungwa mabao matano na kufunga mawili, na wana mchezo mgumu ugenini kwa West Bromwich Albion. Ni hao Albion ambao mwishoni mwa msimu uliopita waliwachakaza Chelsea 3-0.
Imekuwa wiki ngumu kwa Mourinho, ambaye licha ya matokeo mabovu kiasi hicho, amekuwa akizozana na benchi lake la matabibu, hasa baada ya kumshukia daktari wa kikosi cha kwanza, Eva Carneiro na yule wa viungo, Jon Fearn na kuwaondosha kwenye benchi lao. Analalamika kwamba walisababisha wasishinde mechi dhidi ya Swansea kwa kuingia uwanjani kumganga Eden Hazard wakati hakuwa ameumia. Hata hivyo, waliitwa na mwamuzi na walikuwa wakitekeleza majukumu yao.
Mourinho alimtoa nahodha wake, John Terry ambaye ni beki wa kati katika dakika ya 45 tu na kumwingiza Kourt Zouma, na hapo ndipo unaonekana umuhimu wa kusajili beki mwingine, japokuwa tegemeo lao, John Stones wa Everton, anawindwa pia na Man City na Manchester United.
Akitetea uamuzi wa kumtoa Terry, Mourinho alidai kwamba ilikuwa mbinu tu za kimchezo kumtoa Terry, ambaye ilikuwa mara ya kwanza kutolewa uwanjani na Mourinho katika mechi ya Ligi Kuu. Mreno huyo alisema alishaamua kwamba lazima Zouma acheze.
Alisema Terry hakuumia, na hata akiwa benchi alikuwa bado ni nahodha na hakuchukia kwa uamuzi wa kumwondoa kwenye kikosi.
Terry alikuwa na wakati mgumu chini ya makocha waliotangulia, Andre Villas-Boas na Rafa Benitez waliomtupa benchi muda mrefu, kabla ya Mourinho kumrejesha ambapo msimu uliopita alicheza dakika zote katika mechi zote za Ligi Kuu.
ARSENAL WAZINDUKIA KWA PALACE
Katika mechi nyingine Jumapili hii, Arsenal walipambana kuhakikisha ushindi ni
wao licha ya kuwa ugenini kwa Crystal Palace, ambako wachezaji walionesha ari ya ushindi, wakicheza kwa kujiamini.
Mshambuliaji wa kati wa Arsenal, Olivier Giroud alionesha makali yake sambamba na Alexis Sanchez, ambapo Giroud alifunga bao la kwanza dakika ya 16 tu ya mchezo, akiitendea haki pasi nzuri ya Mesut Ozil.
Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika 12 tu, kwani Joel Ward wa Palace alisawazisha kwa majalo nzuri, ambapo kipa Petr Cech wa Arsenal hangeweza kufanya lolote zaidi ya kwenda kuokoka mpira kwenye kamba.
Sanchez aliyetoka mapumziko kwa kushiriki michuano ya Copa America alifanya kazi ya ziada, akiwapa raha washabiki wa Arsenal kwa kasi na maarifa yake, ambapo mashuti yake matatu yaliokolewa kuingia wavuni mapema.
Hata hivyo, jitihada zake zilizaa matunda kwa kusababisha bao la pili, pale mpira wake wa kichwa aliojikunja na kuupiga kwa nguvu kubwa kumparaza Damian Delaney kabla ya kujaa nyavuni kwa Palace wanaofundishwa na Alan Pardew.
Kiungo Francis Coquelin bado alionekana kutokuwa vyema, ambapo alishindwa kuonesha kiwango badala yake akacheza rafu kadhaa na angeweza kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini kocha Arsene Wenger akawa mjanja, akamtoa na kumwingiza Alex Oxlade-Chamberlain.
Viungo Santi Cazorla, Ozil na Aaron Ramsey walionesha ufundi wa aina yake kwenye eneo lao, wakiwaacha vinywa wazi wale wa Palace, ambapo kati ya pasi 55 alizotoa Ozil, ni moja tu alikosea. Kuna wakati walipigiana jumla ya pasi 14, ikiwa ni pamoja na mpira wa kurusha.