Menu
in ,

CHASAMBI AMEKUBALI KUKAA BENCHI ?

Tanzania Sports

Kuna swali ambalo bado hajaulizwa Ladack Chasambi na tunaogopa kumuuliza na kuna wakati mwingine hatuoni umuhimu wa kumuuliza lakini anatakiwa kulijibu swali hili.

Ladack Chasambi ni nani ? Anafahamu akili ya soka aliyonayo ? Anatambua thamani ya madini yaliyopo kwenye miguu yake ? Ni lini ataamua kuhamisha mboni za macho yake na kuziweka kwenye miguu yake ?

Ladack Chasambi anafahamu uhaba uliopo hapa nchini wa vipaji vya wachezaji wanaocheza eneo la kiungo cha mbele ? Ladack Chasambi hasikii hata malalamiko kutoka kwa mashabiki dhidi ya Joshua Mutale ?

Haoni kuwa mashabiki hawajaridhisha na kipaji cha Mzambia huyo ? Hajawahi kufikiria kuwa yeye anakipaji kikubwa kuzidi Mzambia huyo?

Kuna miguu mingi ya kushoto iliyowahi kupita msimbazi, mguu bora wa mwisho wa kushoto ulikuwa wa Luis Jose Miquisone. Baada ya mguu huu kuondoka msimbazi, mguu uliokuwa unashabiana nao ni mguu wa kushoto wa Ladack Chasambi.

Natamani mguu huu ufike katika Kibo ya mlima wa soka kwa bahati mbaya mpaka muda huu ninapoandika mguu huu haijafanikiwa kufika hata Mawenzi.

Tatizo ni nini ? Swali gumu ambalo sina jibu nalo sahihi. Inawezekana wakati Ladack Chasambi alipoanza kupanda mlima soka alikutana na watu waliomwambia hapo alipo ndipo kileleni na akasahau kabisa kilele cha soka kipo Kibo.

Ladack Chasambi amekubali kuwa kichuguu na hakuna anayemkumbusha kuwa kuna siku viongozi watakapoamua kujenga barabara watakiondoa kichuguu kupisha ujenzi wa barabara. Anatakiwa akumbushwe kuhusu hili.

Naandika hivi nikiamini Ladack Chasambi ana nafasi kubwa sana kwenye kikosi cha Lunyasi. Naamini Ladack Chasambi ana mguu wenye sanaa, ubunifu na anaweza kuupa amri mpira na wenyewe ukatii.

Akumbushwe kila uchwao. Akumbushwe kuwa Kariakoo siyo sehemu yake anayostahili kuiweka kama makazi ya kudumu. Kariakooo kwake ni barabara ya kwenda sehemu sahihi kulingana na kipaji chake kikubwa alicho nacho.

Tunaikosea sana Dunia kushindwa kumkumbusha huyu mtoto kuwa pale Msimbazi nafasi yake iko wazi. Anaweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kuzidi mchezaji yoyote pale. Anaweza kufunga magoli mengi kuzidi Joshua Mutale.

Miguu yake inaubongo na ubongo wake una macho wa kuongoza miguu yake. Ladack Chasambi anatukosea sana kushindwa kutupa furaha kupitia miguu yake. Inawezekana amejisahau tumkumbushe.

Bado mapema sana. Tanzania mpaka muda huu tunajilaumu kwanini hatukufanikiwa kukipeleka kipaji cha Ibrahim Ajib kwenye ligi kubwa duniani. Kuna vipaji vingi sana tulivipoteza kwa sababu tulisahau kuvikumbusha kuwa vinaweza kufanya makubwa.

Tumwambie Ladack Chasambi atazame jukwaa la Simba kipindi Joshua Mutale anapokuwa na mpira mguu aone namna ambavyo mashabiki hawaridhiki na kiwango cha Joshua Mutale.

Kiwango ambacho hakizidi kiwango cha Ladack Chasambi. Ladack Chasambi anaweza kufanya maamuzi sahihi akiwa na mpira mguuni kuzidi Joshua Mutale. Ladack Chasambi ni hatari kuzidi umachachali wa Joshua Mutale.

Ni Ladack Chasambi tu kuamua kama anataka kuendelea kukaa benchi au anataka kuwa mfalme wa Msimbazi. Uwezo wa yeye kuwa mfalme anao kabisa tatizo ni kwamba hajaamua.

Kuna wakati ufalme hupiganiwa na siyo kusubiri kupewa. Inatakiwa akae apiganie ufalme. Asiridhike na yeye kuwa Simba hata kama anakaa benchi. Simba siyo kituo chake cha mwisho, Simba ni njia ya kwenda sehemu kubwa.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Leave a Reply

Exit mobile version