Inawezekana kuna maswali mengi sana ambayo yanapita kwenye kichwa chako kuhusiana na kikosi cha Simba kwa sasa. Moja ya swali ambalo unaweza kujiuliza ni mchezaji yupi muhimu na bora kwa sasa kwenye kikosi hiki?
Inawezekana swali lako linaweza likaanzia kwa Aishi Manula? sidhani kama itakuwa sehemu sahihi kwa sababu yeye na Beno Kakolanya hakuna ambaye anauhakika wa kuwa kipa namba moja kwenye kikosi hiki.
Kigugumizi changu kinaweza kuanzia kwa hawa mafahari wawili ambao wanaenda ukuta mahiri wa klabu ya Simba, yani Paschal Wawa pamoja na Erasto Nyoni.
Mabeki wawili imara katika timu, mabeki ambao kila wakikosekana Simba huwa inatetereka sana. Ni mabeki wa kisasa wenye umri mkubwa, pamoja na ukubwa wao kiumri Lakini wanaenda na matumizi ya soka la kisasa (modern football).
Kwanini nasema hivyo? Pascal Wawa na Erasto Nyoni huwa wanacheza high defensive line (hujipanga kwa kukaba katika mstari wa juu). Huwa hawakabii katika mstari wa chini, muda mwingi huwa wanakabia mstari wa juu.
Mahitaji ya soka la sasa huitaji mabeki ambao wanaweza wakakabia juu kama Pascal Wawa na Erasto Nyoni. Unapokabia juu huwalazimisha wapinzani wawe katika eneo Lao muda mwingi.
Pili, soka la sasa huitaji mabeki ambao huanzisha mashambulizi kwa kutokea nyuma. Hili eneo Erasto Nyoni na Pascal Wawa wako vizuri sana kwa sababu huwa wanaanzisha mashambulizi kwa kutokea nyuma.
Wanauwezo wa kuanzisha mashambulizi na kupiga pasi vizuri. Unapokuwa na mabeki wa kati ambao huwa wanaanzisha mashambulizi kutokea nyuma husaidia kupatikana kwa spaces (uwazi) katika eneo la mpinzani kwa sababu mpinzani atalazimika kuja kukaba juu kwake na kuacha uwazi eneo lake.
Inawezekana Jonas Mkude kwa sasa yupo kwenye kiwango kizuri sana, anazuia sana na kuisukuma timu lende mbele. Mara nyingi huwa hataki timu yake ibaki nyuma , mguu wake hulazimisha timu iende mbele.
Kwenda timu mbele siyo tatizo, tatizo huja kwa kiungo ambaye anauwezo wa kuunganisha safu ya kiungo na safu ya ushambuliaji, kwa Simba hapa utamkuta Chota Chama. Huyu ndiye moyo wa Simba akisimama tu kupiga mapigo uhai wa Simba huwa mashakani.
Tete ndiye huunganisha timu, inawezekana hafungi kama Luis Miquissone, John Raphael Bocco, Kahata au Meddie Kagere ila huyu ndiye anayewafanya hawa wang’are.
Ana pumzi kubwa, kasi, uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, utamuona katikati ya uwanja, utamuona pembeni mwa uwanja. Yote haya huyafanya ili kuhakikisha Simba inakuwa na muunganiko kupitia miguu yake ambayo inasimama kama spana ya kuunga nuti za Simba.