Wakati mapato yaliyopatikana katika mechi 26 za mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyomalizika jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita kwa timu ya taifa ya Uganda ‘Cranes’ kuibuka mabingwa yalikuwa ni jumla ya Sh. milioni 267, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa michuano hiyo imewaacha wakiwa na deni la zaidi ya Sh. milioni 200.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa mbali na udhamini wa Sh. milioni 823 walioupata kutoka katika kampuni ya bia ya Serengeti (SBL), pia walipata Sh. milioni 50 kutoka NSSF na PSPF wao waliwapatia Sh. milioni 20.
Osiah alisema pia katika mashindano hayo walipata udhamini wa mafuta yenye thamani ya Sh. milioni 20 kutoka kwa kampuni ya GAPCO kwa ajili ya magari yaliyokuwa yakihudumia timu, viongozi na wageni waliofika nchini kushuhudia michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Michezo la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
“Tunashukuru kuwa hoteli zote tumezilipa, lakini wale waliokuwa wanatoa huduma ya usafiri na mambo mengine bado wanatudai,” alisema katibu mkuu huyo.
Alisema kuwa bajeti kamili ya mashindano hayo ilikuwa ni Sh. bilioni 1.4 na fedha taslimu walizopata kupitia wadhamini na mapato ya milango zilifikia Sh. bilioni 1.2.
Hata hivyo, Osiah alisema kuwa bado Idara ya fedha ya shirikisho hilo kwa kushirikiana na kamati ya fedha ya CECAFA inaendelea kuhakiki matumizi yaliyofanyika ili kuweza kujipanga jinsi ya kuwalipa wote waliowapatia huduma kwa wakati.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kwenye Uwanja wa Taifa na Chamazi yakishirikisha nchi 12, mechi iliyoingiza mapato makubwa ilikuwa ni ya ufunguzi kwa waliokuwa mabingwa watetezi na wenyeji, Kilimanjaro Stars dhidi ya Amavubi ya Rwanda iliyokusanya Sh. milioni 64.1.
Taarifa zaidi kutoka TFF zinasema kuwa hadi hatua ya makundi inamalizika jumla ya Sh. milioni 145. 6 zilipatikana, robo fainali (Sh. milioni 58.4) huku ile ya nusu fainali iliingiza Sh. milioni 55.7 na fainali iliingiza Sh. milioni 17.1.
Mechi iliyoingiza kidogo ilikuwa ni ile iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi ambapo Uganda waliikaribisha Somalia na fedha zilizopatikana zilikuwa ni Sh. 446,000.
Jumla ya washabiki walioshuhudia michuano hiyo walikuwa 103,312. Mashabiki walioshuhudia hatua ya makundi walikuwa 65,617, robo fainali (17,844), nusu fainali (16,014) wakati fainali walikuwa 4,837.