KAMPUNI ya simu za mkononi ya Celtel imetoa Sh120milioni kudhamini mashindano ya golfu katika klabu ya Lugalo ikiwa ni mkataba wa miaka mitatu.
Meneja Uhusiano wa Celtel, Beatrice Singano, alisema jana kuwa kampuni yake ina lengo la kuboresha mchezo huo katika klabu hiyo na pia ni sera ya kuendeleza mchezo huo kwa wazalendo katika klabu hiyo.
Singano alisema kuwa muendelezo wa udhamini wa kampuni yake ndiyo uliyokubali kutoa Sh7milioni kwa ajili ya udhamini wa mashindano ya kimataifa ya golfu inayoanza kesho kwenye viwanja hivyo vya Lugalo.
Beatrice alimkabidhi mfano wa hundi, Katibu Mkuu wa klabu ya gofu, Brigedia Jenerali Julius Mbilinyi.
Beatrice alisema kuwa kampuni yake ina lengo la kudhamini mashindano ya golfu lengo likiwa kuukuza mchezo huo nchini.
Naye Mbilinyi aliipongeza Celtel kwa ofa hiyo na kusema kuwa klabu yake sasa ina uhakika wa kufanya mashindano kwa kuwa ina udhamini imara wa Celtel.
Mashindano hayo yatakayokuwa yakiitwa Celtel Lugalo Open yanayoanza kesho, yatashirikisha washiriki kutoka mkoa wa Arusha pamoja na washiriki kutoka, Moshi, Mufindi, Gymkhana Dar es salaam na wachezaji wenyeji ambao ni kutoka klabu ya Lugalo. Pia Wakenya watashiriki michuano hiyo.
Michuano hiyo itaanza kwa wachezaji vijana na wasichana kabla ya wachezaji wa umri mkubwa pamoja na wachezaji wa kulipwa ambao kampuni ya bia Tanzania, TBL ndiyo itakayokuwa na jukumu la kutoa zawadi kwa wachezaji wa kulipwa. Fainali za michezo hiyo zitafanyika Jumapili.