Safari ndefu ya Arsenal kumpata kipa mkongwe wa Chelsea, Petr Cech hatimaye imetimia baada ya kuingia hatua ya mwisho ya vipimo vya afya vyake ambapo aliwasili kwa Washika Bunduki wa London saa chache zilizopita.
Cech (33) ambaye ni kipa wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech amevuka hatua hiyo baada ya vigingi kadhaa, lakini hatimaye klabu zikakubaliana dau, yeye mwenyewe na Arsenal wakamalizana juu ya mshahara na mengineyo ndipo ametinga kwa vipimo vinavyodhaniwa kuwa utaratibu wa kawaida tu.
Inaelezwa kwamba Cech aliyekuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake Chelsea ameuzwa kwa pauni milioni 11, na amefurahi matakwa yake kusikilizwa na mmiliki wa klabu, Roman Abramovich – kwamba abaki jijini London tofauti na kocha Jose Mourinho aliyetaka auzwe ng’ambo.
Cech amekaa miaka 11 Chelsea na katika historia hiyo anajivunia kutwaa mataji yote waliyoshindania, walau mara moja, kama vile ubingwa wa Ulaya. Abramovich ametaka aachwe achague pa kwenda kama shukurani kwa utiifu alioonesha kwa klabu.
Ametaka kuondoka Chelsea kwa sababu ya kupata muda zaidi wa kucheza, kwani nafasi yake ya kwanza imechukuliwa na Thibaut Courtois. Kuingia kwake Arsenal kunaweza kumaanisha kuanzisha safari nyingine kwa mmoja wa makipa wao, chaguo la kwanza ngwe ya pili ya msimu uliopita, David Ospina au Wojciech Szczesny.
Ospina ni kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Colombia aliyejiunga Arsenal msimu uliopita akitoka Nice ya Ufaransa wakati Szczesny anadakia Poland, akionekana kusukumwa chaguo la pili na kipa wa zamani wa Arsenal, Lukasz Fabianski.
Arsene Wenger atakuwa mwenye furaha kubwa kwa kufanya usajili wa kwanza kiangazi hiki katika jina kubwa kama la Cech, ambapo amekuwa akichagizwa na kutoimarisha eneo hilo kitambo sasa. Atakuwa kifua juu pia dhidi ya hasimu wake, Mourinho, na atasubiri kwa hamu mechi ya Ngao ya Jamii itakayofungua pazia kwa ajili ya Ligi Kuu ya England 2015/16.
Arsenal wanadhaniwa kukubali kumlipa Cech pauni 100,000 hivi kwa wiki, na kumfanya awe kipa anayelipwa vizuri zaidi katika historia ya Arsenal. Awali Washika Bunduki wa London walikaribia kukata tama ya kumpata kutokana na jinsi Mourinho alivyosema, ambapo baadaye alitaka wabadilishane na mchezaji mzawa wa England kati ya Theo Walcott na Alex Oxlade -Chamberlain.
Majadiliano baina ya klabu mbili hizi yamechukua wiki kadhaa na kuhitimishwa mapema kuliko ilivyopangwa awali, kwani ilikuwa apimwe afya yake Arsenal wiki ijayo. Klabu nyingine iliyokuwa ikimhitaji ni Paris Saint Germain.
Wachezaji wengine walioshitua wadau kwa kuhamia klabu hasimu ni Sol Campbell aliyetoka Tottenham kwenda Arsenal 2001, Rio Ferdinand kuwakimbia Leeds hadi Man United 2002, Ashley Cole wa Arsenal kwenda Chelsea 2006 na Carlos Tevez aliyetoka Man United kwenda Man City 2009.
Fernando Torres naye alishitua watu aliposajiliwa na Chelsea kutoka Liverpool 2011 wakati wana Arsena walikasirishwa na nahodha wao, Robin van Persie kuhamia Man United 2012 baada ya kukataa kubaki Emirates, akisema alikuwa akitaka makombe