BAADA ya kuwa katika hatihati ya kutofanyika kwa kukosa wadhamini, michuano ya Chalenji mwaka huu, michuano hiyo imepata udhamini mnono wa dola 350,000 (sawa na shilingi milioni 455) kutoka kampuni binafsi na Serikali ya Kenya.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye alisema jana kuwa baraza lake limeingia mkataba na Kampuni ya Kenya Orange Telecom wa dola 200,000.
Udhamini huo mnono umekuja baada ya Serikali ya Kenya kutangaza kudhamini mashindano hayo kwa dola 100,000 huku Kampuni ya Kenya Broadcast Corp nayo ikitoa dola 50,000.
Mshindi katika mashindano hayo atajinyakulia kitita cha dola 40,000 wakati mshindi wa pili atapata dola 30,000 wakati mshindi wa tatu dola 20,000.
Musonye alisema kutokana na kupata udhamini mzuri msimu huu Baraza lake limeongeza zawadi ya mlinda mlango bora, mfungaji bora, timu yenye nidhamu na mwamuzi bora.
“Lengo letu ni kuwapa changamoto wachezaji wetu wajitume katika mashindano, tunataka mapinduzi ya soka kwenye nchi za ukanda wa Cecafa,”alisema Musonye ambaye akiwa na imani kuwa timu za ukanda huo zitafanya vizuri zaidi msimu ujao katika mashindano ya Shirikisho la Soka Afrikza, CAF.