Carlinhos amekuwa mchezaji maarufu Yanga. Ni kiungo ambaye anaonekana kucheza kimahesabu zaidi. Nyota huyo amecheza mechi mbili za Ligi Kuu kati ya nne, haonekani kuwa na kipaji kikubwa kama Feisal Salum au Haruna Niyonzima.
Carlinhos ni mchezaji wa kipekee kwenye Ligi Kuu si kwa sababu ya ubora bali namna majukumu yanayofanyiwa kazi. Katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara ametengeneza mabao mawili dhidi ya Mbeya City na Mtibwa Sugar.
Mabao yote yametokana na mipira ya adhabu ya kona. Kona aliyochonga katika dakika za lala salama dhidi ya Mbeya City ilitua kichwani mwa Lamine Moro aliyepachika bao safi kwa vigogo hao. Kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, kiungo huyo alipiga kona nyingine iliyotua miguuni mwa Lamine Moro na kupachika bao maridadi kabisa.
Baada ya hapo swali lilinijia; kwanini Carlinhos anaonekana kwenye matukio ya mipira ya adhabu pekee? Mara nyingi tumekuwa na viungo ambao wanatuburudisha muda wote wanaokuwa dimbani. Tumeshuhudia viwango vya viungo wengi klabuni hapo, lakini si wote wanaocheza kama Carlinhos.
Matukio mawili yamempa umaarufu, kana kwamba ni mchezaji maalumu wa kupiga mipira adhabu. Je, Yanga wamewahi kuwa na mchezaji maalumu wa mipira ya adhabu? Hili linatuongezea swali jingine, je klabu zetu zina wachezaji ambao wamegundulika kuwa maalumu wa mipira ya adhabu,penati au kona? Huenda jibu tunalo.
Mwenendo wa Carlinhos unatukumbusha namna wachezaji wawili waliotikisa soka la Ulaya. Nahodha wa zamani England, David Beckham alikuwa mahiri wa upigaji wa mipira ya kona na adhabu. Naye nahodha wa zamani wa Olympique Lyon, Juninho Penambucano alikuwa hodari katika mipira ya adhabu. Hata hivyo wawili hao wanamzidi Carinhos kwa mbali, kwa sababu walishiriki mchezo mzima kwa ustadi. Hii ina maana wapo wachezaji wanaoingia uwajani wakiwa na majukumu maalumu. Wanabeba timu au akuamua mwelekeo wa kila ‘move’ za timu kusaka ushindi. Wengine ndiyo huibuka kama Carlinhos kupitia mipira ya aadhabu.
Nakumbuka tukio moja la kusisimua lilifanywa na Toni Kroos wakati wa mchezo wa El Clasico kati ya Real Madrid dhidi ya Barcelona kwenye dimba la Santiago Bernabeu msimu uliopita. Kroos alipokea pasi kutoka Vinicius Junior baada ya gonga safi kati yake, Benzema na Mendy.
Wakati mpira ukiwa miguuni Kroos aliinua mkono kutoa maelekezo mahali anakotaka timu ipite kuelekea lango la Barcelona. Aliwaangalia Vinicius na Benzema kisha mkono ukatoa maelekezo kwamba Vinicius amzunguke Semedo kuelekea eneo la hatari. Ishara ya mkono ule ndiyo ilikuwa maarifa makubwa ya kiungo huyo Mjerumani.
Vinicius alionekana kama mwanafunzi mbele ya mwalimu aliyekuwa akielekeza nini cha kufanya ili kuleta matokeo chanya. Vinicius alichomoka kadiri alivyoelekezwa ndipo Kroos akapitisha pasi kwenye eneo lile lile aliloekeza, na Vinicius hakufanya makosa, akatuliza mpira kisha kupiga shuti lililojaa kimyani.
Gerard Pique alijaribu kuteleza kuzuia shuti lile, ikashindikaka. Ter Stegen pale lango hakuwa na la kufanya wakati mpira ulipopita begani mwake na kujaa wavuni.
Kwanini nasema hivi? Toni Kroos ndiye anapanga namna ya kushambulia lango la adui. Anaamua timu icheze vipi, na wakati gani ielekee upande wa kulia au kushoto. Anaelekeza iwe katikati,pembeni kulia na kushoto au kurudisha mpira nyuma ili kuanza upya kutengeneza shambulizi. Hapo ndipo likaanza jina la ‘Toni PhD’. Lakini Toni ni mzuri pia katika mipira ya kona, anachonga vizuri, ana muono wa mbali na namna anavyoweza kutengeneza mawasiliano yake na wenzake. Ni suala la kiufundi zaidi.
Iwe Ligi Kuu Tanzania Bara ama kwingineko timu zinahitaji viungo wabunifu. Viungo ambao wanaleta mbinu mbadala, kwamba kocha anahitaji ubora wa mchezaji fulani katika mchezo kwa sababu ana ubunifu wa aina fulani. Si kila mbinu za kocha zinaweza kuwapa nafasi wachzaji wote kutumika, lakini wapo wanaoweza kutumikia mbinu kwa vikle wanaongeza kitu cha ziada.
Eneo la ushambuliaji pia liko hivyo, anahitajika mshambuliaji ambaye ataongeza kitu cha ziada baada ya mbinu za kocha. Ushindi wa mchezo hauishii kwenye mbinu za kocha bali uwezo wa wachezaji kutumikia mbinu hiyo wanapokuwa na kitu cha ziada; mfano kubadilika, ubunifu,maarifa wakati wa mchezo,kujituma,ushirikiano na mengineyo.
Viungo wabunifu ni miongoni mwa wachezaji wanaopendwa na timu zinazocheza soka la pasi nyingi. Wachezaji wa aina hiyo huwa wanatoa ubunifu, kuanzia chenga,utoaji wa pasi za mwisho,kutengeneza mabao na uwezo wa kushirikisha mabadiliko ya mbinu za mwalimu wakati mchezo unapoendelea.
Abdi Kassim Babi alikuwa mahiri katika upigaji wa mashuti. Yeye alikuwa mchezaji ambaye anapopata nafasi kwenye kumi na nane huachia makombora makali.
Mara nyingi alipachika mabao ya namna hiyo. Uwezo wa kupiga mashuti haufundishwi na kocha pekee, bali mchezaji mwenyewe amejaliwa ufundi huo ambao unamsaidia kocha kuimarisha kikosi chake kwa kuamua amtumie namna gani.
Eneo hilo pia alikuwa Joseph Kaniki mwenye nguvu kama Sarpong wa Yanga na umahiri wa kupachika mabao ulitokana na maarifa yake ya kutumia nguvu na mashuti makali dhidi ya mabeki.
Emmanuel Gabriel alikuwa mchezaji hatari kwenye boksi la adui. Ni mshambuliaji ambaye alikuwa ana anatumbikiza mipira wavuni kwa sababu ya nguvu au mashuti bali uwezo wa kujipanga na kujiweka katika nafasi ya kupachika mabao. Uchezaji wake sawa na Filippo Inzaghi.
Carlinhos kama ilivyo kwa Feisal Salum ni viungo wanaohitaji kulindwa na kiungo mkabaji. Ni wapishi na wana macho ya kiufundi. Wanamhitaji zaidi Mukoko ambaye atawalinda kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho.
CARLINHOS ANAFAA WAPI?
Kumtegemea Carinhos katika mfumo wa 4-4-2 imekula kwako. Ukimtegemea Carlinhos kwenye mfumo wa 4-2-3-1 utalamba bingo, kwa sababu atakuwa na viungo wawili pembeni mwake; mmoja akiwa kiungo mlinzi Mukoko Tonombe, halafu anakaribiwa na Feisal Salum, kwa maana Carlinhos hatakuwa na jukumu la kuchangia ulinzi, yeye anafaa kukabidhi pasi timu inaposaka goli.
Hii ina maana kocha wa Yanga anatakiwa kupanga mshambuliaji mmoja katika mfumo wa 4-5-1, ili kuwezesha kuwa na viungo wawili wa ulinzi watakaohakikisha kazi za Feisal Salum na Carlinhos zinakwenda vizuri. Na kwa vile Haruna Niyonzima anamudu kucheza upande wa kulia, basi mshambuliaji wa pili nyuma ya Sarpong anaweza kuwa Carlinhos.
Kazi ya Carlinhos si kukaba, hashughuliki na kukimbiza na wapinzani wanaoshambulia Yanga. Badala yake Carlinhos anaonekana kufaa zaidi pale timu inaposhambulia na kutengeneza nafasi za kufunga,kutafuta makosa ya wapinzani(adhabu za kona,penati na nyinginezo).
Carlinhos na Tonombe ni wachezaji wa kati wanaofahamu wapo pale kwa ajili gani. Tunapopata mpira lazima kumtazama mshambuliaji si kupiga chenga,kanzu, na madoido ambayo mwisho wa mchezo hayajazalisha ushindi. Carlinhos hafanyi mambo mengi, wala kukupa mengi lakini yana umuhimu yale anayokupa uwanjani; ni matokeo.