Wawakilishi wa Afrika wameshindwa kulinda heshima ya bara lao kwa kupoteza mechi ya kwanza muhimu kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Cameroon waliepushwa kufungwa mabao mawili ambayo yalikataliwa na mwamuzi katika kundi A la michuano hiyo, lakini wakaruhusu bao jingine na kuzama.
Mexico walikataliwa mabao mawili mapema kiutata kutokana na jitihada za Oribe Peralta na Giovani Dos Santos.
Pamoja na malalamiko ya wachezaji wa Mexico, Cameroon hawakuwa tishio sana lakini Samuel Eto’o alikaribia kufunga lakini shuti lake likagonga mwamba huku mpira wa adhabu wa Benoit Assou-Ekotto ukitoka nje.
Mexico walifarijika kwa mkwaju wa Dos Santos kupanguliwa kidogo kabla ya Peralta kuwasili na kukwamisha mpira wavuni.
Nusura Cameroon waondoke na pointi moja katika dimba la Estadio das Dunas jijini Natal dakika za mwisho pale mpira hatari wa kichwa wa Benjamin Moukandjo ulipookolewa kisarakasi na kipa Guillermo Ochoa.
Mexico walicheza vizuri zaidi ya Cameroon kwa ujumla ambapo walipanga vyema mashambulizi yao na huenda wakawatisha wenyeji Brazil Jumanne.
Peralta sasa amefunga mabao saba katika mechi nne za kiushindani, huku ufanisi wa Cameroon ukiwekwa shakani, ikizingatiwa uwezo wa Croatia na wenyeji Brazil.
Kimsimamo sasa Cameroon ni wa tatu, nyuma yao wakiwa Croatia ambao hata hivyo ni wakali, wa kwanza wakiwa Brazil wanaofuatiwa na Mexico katika kundi lao A.
Cameroon walipata tabu ya kuwakabili Mexico waliocheza kwa mfumo wa 5-3-2. Cameroon walikuwa na matatizo nyumbani, kwa kugoma kupanda ndege kwa sababu ya kutolipwa posho kabla ya mambo kuwekwa sawa.
Eto’o pia inaelezwa alichezeshwa licha ya kutokuwa vyema kwa kiwango chake kutokana na matatizo ya afya.
Ushindi wa Mexico ni wa kwanza dhidi ya timu ya Afrika kwenye mashindano ya fainali za Kombe la Dunia. Cameroon wameshinda mechi moja miongoni mwa 14 zilizopita katika michuano hii.
Cameroon walipiga mashuti 13 dhidi ya wapinzani wao waliopiga tisa, lakini ni moja tu lililolenga goli na lilikuw akatika dakika ya 90, hivyo wanahitaji kuwa makini zaidi kwenye mechi mbili zilizobaki katika kundi lao dhidi ya Brazil na Croatia.
Francisco Javier Rodriguez wa Mexico aliongoza kwa kutoa pasi 74, akimzidi aliyeongoza kwa upande wa Cameroon kwa pasi 38.