Ni kama vile kizazi cha makipa kilipotea kabisa, ambako mara ya mwisho makipa kama Andre Arentes (Afrika kusini), Vincent Enyeama (Nigeria) na Tony Sylva (Senegal) walionesha umahiri mkubwa sana zama zao…
NAFASI ya golikipa mwenye mafanikio barani Afrika iliikuwa finyu sana. maeneo mengine yaliyoonesha wachezaji wake kutamba ni mabeki w a pembeni na kati, viungo, mawinga na washambuliaji. Ukiangalia nafasi ya mawinga Afrika imeshuhudia viwango vya akina Finidi George (Nigeria), Olembe (Cameroon), Tijjan Babangida (Nigeria) na wengineo miaka ya zamani. Mustapha Haji (Morocco), Jaziri (Tunisia) na wengineo. Nafasi ya golikipa haikuwa tishio miaka ya karibuni hadi alipoibuka Eduardo Mendy raia wa Senegal. Hata hivyo nyota huyo ameishi na kukulia nchini Ufaransa.
Ni kama vile kizazi cha makipa kilipotea kabisa, ambako mara ya mwisho makipa kama Andre Arentes (Afrika kusini), Vincent Enyeama (Nigeria) na Tony Sylva (Senegal) walionesha umahiri mkubwa sana zama zao. Vile vile imewahi kutokea makipa wenye makosa mengi kama Peter Rufai (Nigeria) ama Hans Vonk (Afrika kusini). Mastaa wengi walioibuka Ulaya na kutamba kisoka ni wale waliocheza nafasi nyingine. Lakini kwa makipa imekuwa adimu. Katika karne ya 21 tangu ilipoanza mwaka 2000 ni makipa wawili walichomoza kwenye vilabu vya Ulaya, Vincent Enyeama, Tony Sylva na Carlos Idrisa Kameni. Makipa si wengi Ulaya, na waliopo wamekuwa wakicheza timu za madaraja ya chini. Kwa miaka ya karibuni majina mawili ndiyo yamechomoza, Andre Onana na Eduardo Mendy. Tofauti ya wawili hawa, Andre Onana amezaliwa na kukulia Cameroon, wakati Eduardo Mendy amezaliwa na kukulia Ufaransa ila kwao Senegal.
TANZANIASPORTS katika tathmini yake imebaini kuwa eneo la makipa limepata nguvu mpya, kwa usajili uliofanywa na Manchester United. Usajili ambao umeibua mjadala juu ya nafasi ya makipa katika vilabu vikubwa barani Ulaya. Mbali na historia iliyopita bado eneo la makipa limekuwa adimu kuchomoza, huku wengi wao wakicheza Ligi za nyumbani Afrika. Tathmini hiyo inaonesha kuwa Cameroon ndilo taifa pekee lenye mafanikio katika nafasi ya makipa kuliko mengine barani Afrika. je ni makipa gani wa Cameroon waling’arisha nchi yao na kuacha urithi zaidi?
ANDRE ONANA
Ana umri wa miaka 27 sasa. Ni mlinda mlango aliyeanza kucheza soka nchini kwao Cameroon, kabla ya kwenda kujiunga na Barcelona akiwa La Masia. Nyota ya Andre Onana ilianzia kwenye kituo cha soka cha Samuel Eto’o na saa amesajiliwa na mabingwa wa zamani wa EPL, Manchester United. Usajili wa Onana unamfanya kuwa golikipa ghali namba tatu kati ya waliopo sasa, ambapo amenunuliwa kwa kiasi cha pauni Milioni 47 akitokea klabu ya Inter Milan ya Italia. Kipa ghali kwa sasa ni Kepa Arrizabalaga aliyenunuliwa kwa pauni milioni 72 na Chelsea. Namba mbili ni Allison Becker wa Liverpool aliyenunuliwa kwa pauni milioni 67.
CARLOS IDRISA KAMENI
Kama unazungumza golikipa toka Afrika ambaye alikuwa anapangua michomo hatari basi huyu alikuwa hodari. Kameni ni mzaliwa wa Cameroon ambaye soka lake lilianzia klabu ya Le Harve ya Ufaransa kabla ya kwenda Saint Etienne. Kiwango chake kikubwa kilichomfanya awe kipa namba noma kilionekana katika timu za Espanyol na Malaga. Kwa miaka 13 ya soka alichezea vilabu hivi nyakati tofauti. Pale Malaga alikuwa panga pangua ndiye anaimama kwenye eneo la kipa. Vilevile Malaga nako ilikuwa panga pangua asingekosekana kikosini. Ukisema kupangua michomo ya ana kwa ana basi huyu ndiye alikuwa kiboko ya washambuliaji wakali wa mashuti. Naye aliwakilisha vizuri taifa lake la Cameroon. Baadaye alihamia klabu ya Fenerbahce ya Uturuki, ile aliyochezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.
JACQUES SONG’OO
Golikipa huyu kama walivyo kawaida ya wakali kutoka Cameroon naye alitamba katika timu mbalimbali Ulaya. Alianzia kuwa nyanda wa klabu ya Toulou, kabla ya kujiunga na Le Mans kisha Metz zote za nchini Ufaransa. Maisha ya Ufaransa hayakuwa mwisho, badala yake alisonga mbele kutua Ligi Kuu Hispania maarufu kwa jina la La Liga. Akiwa nchini Hispania alijiunga na klabu ya Deportivo Coruna ambayo enzi zao ilikuwa kali na ilitetemesha vigogo. Naye aliwakilisha vema bendera ya Cameroon katika nafasi ya makipa.
JOSEPH ANTOINE BELL
Mwamba uliotetemesha soka la Afrika na baadaye akaelekea kucheza barani Ulaya. Bell aliondoka Afrika kuelekea klabu ya Olympique Marsaille ya Ufaransa. Klabu ambayo ilimlea na kukuza kipaji cha Zinedine Zidane. Mareseille ndiyo klabu aliyochezea pia kiungo machachari Abedi Ayew ‘Pele’ wa Ghana baba mzazi wa Jordan Ayew na Andre Ayew. Bell aliichezea Marseille kwa umahiri na kupeperusha vema bendera ya Cameroon kisha akaelekea klabu zingine za Toulou,Bordeaux na Saint Etinne, zote za Ufaransa. Jina lake katika viwanja vya soka Ufaransa linakumbukwa kwa uwezo mkubwa na kuwa miongoni mwa manyanda waliotikisa soka Ulaya.
THOMAS NKONO
Ukitaka kujua umahiri wa mwamba huyu basi mtafute Gianluigi Buffon, Yule nyanda hatari wa Juventus na timu ya Taifa ya Italia. Mwaka 1990 Buffon alikuwa muokota mipira kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika kwao Italia. Katika fainali hizo Cameroon ilitikisa soka kwa kumwachapa mabingwa watetezi Argentina kwa 1-0. Langoni mwa Cameroon alikuwa amesimama imara Thomas Nkono. Kwenye fainali hizo Cameroon walitinga hatua ya robo fainali kabla ya kung’olewa na England. Umahiri wa Thomas Nkono ndiyo ulimfanya Buffon ampatie jina la Thomas mtoto wake wa kiume. Ni kama zawadi kwa Thomas Nkono aliyekuwa kiboko ya washambuliaji. Nkono alikuwa akichezea klabu ya Espanyol yenye makao yake katika jimbo la Catalonia, sambamba na Barcelona nchini Hispania.
Yeye ndiye mbabe wa kwanza kuwakilisha vema Cameroon langoni. Ndiye aliyejenga ushawishi kwa makocha kuwaamini makipa wa Cameroon hadi sasa Andre Onana anakuwa mlinda mlango namba moja wa Manchester United. Hakuna kipa wa kutoka bara la Afrika aliyewahi kuichezea Manchester United. Hapa msomaji usilete jina la Gary Bailey, aliishi Afrika kusini na wazazi wake ila yeye ni mzaliwa wa England na alikipiga muda mrefu Man United. Andre Onana anawakilisha Cameroon na kuthibitisha kuwa miundombinu ya walimu na huduma bora ya elimu ya soka italeta mapinduzi makubwa.