Cameroon nje Kombe la Mataifa Afrika
Siku ya pili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika imeacha watu vinywa wazi.
Moja ya maajabu ya Jumapili yalikuwa Cape Verde kuwang’oa katika mashindano Cameroon waliopata kufika robo fainali ya Kombe la Dunia.
Vijana wa Cape Verde waliokuwa wakionekana wasindikizaji tu, waliwaaibisha Cameroon na kufuzu kwa mara ya kwanza kuingia fainali hizo zitakazofanyika Afrika Kusini Januari mwakani.
Cape Verde wamewang’oa Cameroon kwa jumla ya mabao 3-2. Cape Verde ni nchi ya visiwa vidogo, yenye watu 500,000 tu.
Vijana hao waliingia uwanjani jijini Younde baada ya kushinda kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Estádio da Várzea mjini Praia mwezi uliopita.
Wakiwa ugenini, Cape Verde waligangamala, na kuishia kufungwa mabao 2-1, hivyo kutinga kwenye fainali hizo kwa wastani wa mabao 3-2, wakiwaacha washabiki wa Cameroon hawaamini kilichotokea.
Cape Verde walitarajia upinzani mkali kutoka kwa Cameroon tangu mwanzo, lakini alikuwa mchezaji anayekipiga Ureno, Heldon Ramos aliyetikisa nyavu za Cameroon dakika ya 22 na kuwapa deni kubwa Simba hao.
Cameroon walikuwa kama nyuki waliochokozwa, wakasawazisha bao hilo dakika chache baadaye kupitia kwa Achille Emana, lakini bado walihitaji mabao zaidi ili kulipa nakisi kubwa.
Hata hivyo, huo ulionekana mtihani mkubwa kwao, kwani licha ya kufurukuta, walipata bao moja tu na hawakuweza kupenya tena ngome ya Cape Verde.
Wenyeji walipata bao la pili dakika nne kabla ya kipenga cha mwisho, kupitia kwa chipukizi mwenye umri wa miaka 16, Fabrice Olinga aliyepokea majalo ya mkongwe, Samuel Eto’o.
Kurejea kwa Eto’o, mchezaji bora wa Afrika mara nne na kubadilishwa kocha kabla ya mechi ya marudiano kuliisaidia kidogo tu Cameroon, lakini dawa haikupatikana.
Katika msingi huo, Cameroon hawatakuwapo Afrika Kusini kwenye fainali za mwakani, ikiashiria kwamba zama za kuwa na fulani fulani kila mara kwenye mashindano zimepita.