Menu
in , , ,

Cameroon: Kashfa kupanga matokeo

Yametolewa madai kwamba wachezaji kadhaa wa Cameroon wamehusika na kashfa ya kupanga matokeo ili timu yao ifungwe.

Kamati ya Maadili ya Chama cha Soka cha Cameroon (Fecafoot) imeanza uchunguzi juu ya taarifa za kashfa inayohusisha wachezaji wake saba.

Cameroon walipoteza mechi zao zote tatu za makundi na kutolewa kwa aibu kwenye fainali ya Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Brazil.

Udanganyifu huo unadaiwa kutumika katika mechi zote tatu za kundi A dhidi ya Brazil, Mexico na Croatia.

The Indomitable Lions walionekana kuwa simba wanaoweza kukatwa si tu sharubu au mkia, bali hata shingo kilaini ambapo katika mechi moja Alex Song alitolewa nje kwa mchezo mbaya na wa kijinga.

Alimpiga Mario Mandzukic wa Croatia akiwa hana mpira huku Wacameroon wengine, Benoit Assou-Ekotto akipigana na Benjamin Moukandjo kwenye mechi hiyo hiyo.

Madai ya kashfa hiyo yalitolewa na Wilson Raj Perumal aliyepata kutiwa hatiani kwa kupanga matokeo na aliyekuwa rumande ya polisi nchini Finland Aprili kwa waranti iliyotolewa na polisi wa kimataifa.

Raia huyo wa Singapore alitabiri matokeo dhidi ya Croatia na kwamba mchezaji mmoja angetolewa kwa kadi nyekundu na kweli ikawa hivyo. 

Watu wamekuwa wakicheza kamari kwa kuweka dili wakitabiri matokeo, kumbe huwa wameshazungumza na wachezaji na kupanga nao wafanye ‘ujinga’ ili waachie mabao ambapo wachezaji hupewa kitita kikubwa cha fedha kwa kuangusha timu zao. Imetokea Uingereza na hata kwenye michuano ya Ulaya.

Cameroon walikuwa wanaogopewa sana duniani enzi za Roger Milla, Cyril Makanaky kwa uzalendo wao, kujituma na kutoendekeza tamaa ya fedha, licha ya kwamba wachezaji wa sasa wanalipwa mamilioni ya dola katika ligi za ng’ambo wanakocheza.

Taarifa ya  FA ya Cameroon inasema: “Tuhuma za udanganyifu juu ya wachezaji wa Cameroon katika michezo mitatu ya awali ya Kombe la Dunia la Fifa 2014, hasa ule wa Cameroon dhidi ya Croatia.

“Pia juu ya kuwapo wachezaji saba waovu kwenye timu yetu ya taifa si taathira ya tunu na misingi inayokuzwa na utawala wetu, kuendana na mfumo wa Fifa na maadili ya nchi yetu.

“Tumejizatiti kutumia njia zote zinazotakiwa kupata suluhu ya suala hili linalovuruga katika muda mfupi kwa kadiri inavyowezekana.”
Fifa imesema haitaki kuvuruga uchunguzi wowote ila kwamba kwa ujumla uadilifu ndicho kipaumbele cha Fifa hivyo inachukulia tuhuma za kupanga matokeo kwa umakini mkubwa.

Perumal katika kitabu chake kilichochapishwa Aprili amesema aliweka mpango na wachezaji wa timu fulani wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing kuhakikisha wanafungwa kwenye mechi mbili za mwanzo.

Jamaa huyo pia alipindisha matokeo kwenye hatua za kufuzu kwa timu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.

Ushiriki wa Cameroon nchini Brazil mwaka huu uligubikwa na giza tangu awali, kwani wachezaji waligoma kupanda ndege wakilalamikia posho kiasi kwamba walichelewa kufika Brazil.

Walianza kwa kufungwa 1-0 na Mexico, kisha wakapoteza kwa Croatia kabla ya kulambwa 4-1 na wenyeji Brazil.

“Baadhi ya wachezaji walionesha tabia mbaya sana, na ndiyo maana tumefungwa mabao manne. Najua ni vigumu kucheza tukiwa 10 lakini hiyo si sababu ya kufungwa kiasi hiki.

Mechi ilikuwa ya uwiano sawa hadi kadi nyekundu ilipotolewa. Croatia walijituma sana mbele ya goli, Cameroon pia tulipata fursa na tulitakiwa kufunga. Tabia za baadhi ya wachezaji kwa kweli haziridhishi hata kidogo, hata tulipokuwa watu 11 kila timu, haikubaliki,” alisema kocha wa Cameroon, Volker Finke baada ya kufungwa na Croatia.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version