Hatimaye Desemba 31 imefika na utekelezaji wa sheria na kanuni mpya uaanza kwenye soka hapa Uingereza.
Hii ni baada ya mchakato mrefu na tata wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU), mchakato uliogharimu hata wakuu kisiasa.
Naam BREXIT itaanza kuathiri klabu na wachezaji juu ya usajili na ufanyaji kazi nchini Uingereza.
Makali yake yanaanza kuonekana kwenye Dirisha Dogo la Usajili Januari hii ambapo mfumo mpya wa Uhamiaji utaathiri jinsi klabu zitakavyoweza kuchukua na kuingia mikataba na wachezaji wa Ulaya na ng’ambo ya hapo.
Ilivyo ni kwamba tangu Desemba 31 mwaka jana, yaani juzi, uhamaji na uingiaji huru wa watu katika Eneo la Uchumi la Ulaya (EEA) na raia wa Uswisi umekoma.
Klabu, kwa maana hiyo, zinatakiwa kufuata matakwa ya sheria na kanuni mpya.
Pamoja na vigezo vipya vya Shirikisho la Soka (FA), tafsiri yake ni kwamba klabu zinakabiliwa na wakati ngumu zaidi katika kufanya michakato ya uhamisho wa wachezaji na kuwasajili kutoka nje ya Uingereza na Jamhuri ya Ireland.
Sasa ili kumnunua na kumsajili mchezaji kutoka huko nje, inahitajika kuwa na leseni maalumu ya michezo ya udhamini.
Kabla ya mchezaji kuweza kuomba visa lazima klabu iwe imeshapata kibali fulani kutoka FA. Kisha hapo ile leseni maalumu itatolewa ikiwa na aina mbili za visa – moja ya muda mfupi wa hadi miezi 12 na nyingine ya hadi miaka sita, kukiwapo uwezekano wa kuruhusiwa makazi ya kudumu nchini baada ya ukaazi wa miaka mitano.
Klabu zilizo nje ya madaraja manne makubwa ya soka kwa wanaume au nje ya mawili makubwa ya wanawake haziwezi kupata leseni hiyo maalumu ya udhamini.
Kuanzia Januari hii FA itatoa kibali maalumu tajwa huko juu moja kwa moja pasipo mchakato kwa wachezaji waliochezea timu za taifa zenye kiwango fulani cha juu na wawe wamecheza kwa muda fulani pia.
Kigezo kingine kwa wachezaji wa nje kusajiliwa ni kuhakikisha kiwango cha juu cha ligi ya klabu inayomuuza, idadi ya dakika alizocheza mwanasoka husika na jinsi klabu ilivyofanya vyema katika mashindano ya ndani na ya bara husika kwa msimu tangulizi.
Wachezaji chipukizi chini ya umri wa miaka 21 wanaweza pia kutathminiwa kuendana na ufanisi wao katika vikosi vya timu za vijana pia.
Katika kuomba kutakuwapo ada ya pauni 500 na VAT.
Klabu zaweza kukata rufaa kwa jopo maalumu Januari hii kwa ada ya pauni 5,000 na VAT ikiwa hawakuridhika na uamuzi wa kuwakatalia wachezaji waliowaweka katika mchakato wa usajili na kukataliwa.
Kwa hiyo sasa, klabu na wafanyakazi wanaohusika na usajili, kabla ya kumleta mchezaji lazima wafanye utafiti kubaini iwapo anakidhi vigezo na masharti ili kuepuka kupoteza muda na gharama.