Menu
in

Brendan Rodgers ni wakati wake sasa  

Brendan Rodgers

Brendan Rodgers

Je, unaweza kumpenda kocha peke yake bila timu anayofundisha? Hilo  ndilo limewahi kunikuta mimi kila nilipotazama timu inayofundishwa na  Brendan Rodgers. Kaa kitako msomaji nikusimulie sababu za kupenda  ufundishaji wa Brendan Rodgers. 

Kwanza ni kocha ambaye kwa sasa anahusishwa na mpango wa kuajiriwa  kufundisha Manchester United. Kuajiriwa kwenye timu kubwa na yenye  historia kabambe kama Manchester United ni sifa kubwa na inampa nafasi  ya kuonesha umahiri zaidi.  

Kama ningekuwa mshauri wa Manchester United ningewaambia  wamchukue kocha huyu na ninazo sababu nyingi mno na anamzidi Ole  Gunnar Solskjaer kwa mbali sana.  

Miaka kadhaa iliyopita Brendan Rodgers alikuwa anafundisha Swansea  City. Kabla ya ukocha wake hapo alikuwa mwanafunzi wa kocha gwiji Jose  Mourinho kipindi alichokuwa akiinoa Chelsea.  

Kwahiyo Brendan Rodgers amejifunza ukocha nje ya darasa kupitia Jose  Mourinho mbali ya vyeti vyake halisi. Mourinho alipoondoka Chelsea  alikuja kuzinoa Inter Milan, Real Madrid, Manchester United na  Tottenham Hotspurs.  

Kwangu mimi Rodgers ana kitu cha aina yake, ni mwalimu ambaye  anafundisha soka ninalopenda. Timu icheze kwa pasi fupi fupi kwa kasi,  kutawala mchezo na kupata ushindi. Yaani timu iwe inacheza soka la  kutafuta pointi au ushindi huku ikiwa inawapa burudani.  

Si kama anavyofundisha Pep Guardiola pasi zinakuwa nyingi wakati  mwingine unaona wazi mipango yake inafeli na haiwezi kumleta pointi.  Kwa Brendan Rodgers nilipenda namna alivyoifanya Swasea City itandaze  soka maridadi na kwa hakika ilikuwa timu inayovutia kuitazama. 

Kuna wakati makocha wanatuvutia sisi mashabiki kutazama timu zao  namna zinavyocheza,kusaka ushindi na burudani anuai. Wakati akiwa  kocha wa Liverpool kulikuwa na presha kubwa ya kutwaa ubingwa.  

Na makosa ya nahodha wao Steven Gerard kwenye mchezo dhidi ya  Cheslea ya Mourinho yakamkosesha taji Brendan Rodgers. Liverpool ilikuwa inacheza soka maridadi,pasi nyingi,kutawala mchezo na ushindi  wake ulikuwa unavutia.  

Timu ya Brendan Rodgers inacheza kwa ari mno, uchu wao wa kupata  ushindi unakuwa umepangiliwa na namna timu inavyojijenga na kuwa  tishio ndipo ninapoona umahiri wa kocha huyo. Anafundisha mpira ambao  unawapa wachezaji nafasi ya kupumua.  

Kwa ufundishaji wake hana kasi ya mchezo muda wote lakini timu zake  huwa zinavutia kuzitazama. Alipokuwa kocha wa Celtic ya Uskochi nako  alikuwa na mtindo uleule kuhakisha timu inacheza kandanda safi na kupata  ushindi ukiwa umewakosaha mashabiki.  

Wakati fulani niliwahi kuandika kwenye moja ya kolamu zangu za  Madridista kuwa natamani siku moja Brendan Rodgers angekuja kuwa  kocha wa Real Madrid.  

Niliamini ni kocha ambaye ana kila sifa za kufundisha timu kubwa ikiwa  ataachiwa utulivu na kupewa muda wa kutosha kwenye hizi timu kubwa.  Presha ya timu kubwa wakati mwingine zinawaumiza makocha hivyo  baadhi hukaa muda mfupi kabla ya kufukuzwa.  

Mtazame Julen Lopetegui wa Sevilla alivyotulia na timu na huwezi kudhani  ndiye kocha aliyefukuzwa Real Madrid. Mtazame Emery Unai alivyotulia  Villareal huwezi kudhani ndiye aliyeondoka PSG an Arsenal. Kwahiyo kwa  Brendan Rodgers kupewa kibarua cha Manchester United, binafsi  natamani mno kumwona akiwa timu kubwa zaidi ya Liverpool iliyoko  kwenye wasifu wake (CV). 

Kwa sasa anao uzoefu wa kufundisha timu za aina mbili; kwanza timu  zenye bajeti kubwa na wachezaji wakubwa na timu ndogo zenye bajeti  ndogo lakini zikafanya mambo mazuri. Kuifundisha Swasea City si sawa na 

Liverpool wala Leicester City si sawa na Celtic au kama atapewa  Manchester United. Kwa bajeti Liverpool ni zaidi ta Celtic,Leicester na  Swansea.  

Tangu alipoichukua Leicester City ameifanya timu hiyo kuwa ngumu,yenye  utulivu na kucheza kwa mipango ambayo inaonekana wazi. Kuna wakati  unaweza kusema anakosa wachezaji wenye vipaji vikubwa au bajeti kubwa  ya kusajili wachezaji.  

Kwa wachezaji alionao ndio ametwaa taji la FA na Ngao ya Jamii. Ni kocha  ambaye amemsumbua Pep Guardiola na mastaa wake ambao walishindwa  kufurukuta mbele ya Leicester City kwenye fainali ya FA. 

Rodgers ana miaka 48 tu na dhahiri muda anao na uchu wa kushinda  mataji bado anao. Kwahiyo kama Manchester United hawana kisingizio  kingine zaidi ya kumpa timu mtu huyu na kumwondoa pale King Power  stadium. 

Furaha ya Brendan haitakuwa kuifundisha Manchester United tu bali  kuona kocha huyo hatimaye maono yangu kuwa anastahili kupewa klabu  kubwa na ambayo alitakiwa kuipata mapema kabla ya Ole Gunnar  Solskjaer.  

Matamanio yangu ni kuona anazinoa timu kubwa kutokana na umahiri  wake kwenye mchezo huo. Ni mapenzi kwake lakini timu pekee ambayo  natamani angekuwa nayo ni Real Madrid tu, kwanza anajua kvaa suti,  ametulia, hana mengi nje ya uwanja,hana kelele kwenye vyombo vya  habari, sio mtengeneza habari kama walivyo makocha wengine maarufu.  Kifupi ametulia mno, ukiongeza na uwezo wake wa ufundishaji unavutia  mno ingawa sio kila wakati unaweza kuipatia taji timu yake.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version