Menu
in

Borussia Dortmund mikononi mwa Marco Rose

Marco Rose

Marco Rose

“Marco anaweza kupata kazi ya ukocha katika klabu yoyote na anaweza kufanya kazi vizuri popote. “ Hiyo ilikuwa kauli ya kocha wa Liverpool Jurgen Klopp aliyotoa mwaka 2019. Katika kipindi hicho Marco Rose alikuwa kocha wa Red Bull Salzburg ya Austria akiwa amefanikiwa kutwaa mataji mfululizo. 

Miaka miwili baadaye Marco Rose anajiandaa kuwa kocha mpya wa klabu ambayo ilifundishwa na Jurgen Klopp ambaye kwake ni shujaa wake. Baada ya kuacha kazi Salzburg wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2019 Marco Rose aliteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Borussia Monchengladbach, ambayo ameiongoza kufuzu hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya. 

Kwenye hatua hiyo Gladbach ilipangwa kupepetana na Man City. Hata hivyo hadi sasa kocha huyo anajiandaa kuchukua kibarua cha kuinoa Dortmund baada ya kuthibitishwa hilo mapema mwezi Februari kwamba atakuwa Iduna Park kuanzia msimu 2021-2022 na kuendelea.

Tangu kuondoka kwa Jurgen Klopp Dortmund mwaka 2015, wamefanikiwa kutwaa mataji ya DFB Pokal mara moja tu na kumaliza BundesLiga wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich katika misimu mitatu. Dortmund ni kama wameshindwa kurudia mafanikio ya Klopp ambaye kwa sasa anainoa Liverpool

Marco Rose anatarajiwa kutua Kaskazini mwa Rhine Westaphalia na kuwa kocha wa sita kukalia viti vya Signal Iduna Park tangu kuondoka kwa Klopp. Lakini Marco anaonekana kuwa kocha anayeweza kuleta mafanikio kama nyakati za Klopp. Rose alikuwa mchezaji katika kipindi cha Klopp pale Mainz alipoanzia ukocha. 

Ni Klopp ndiye aliyemsajili kwa mkopo kutoka klabu ya Hannver ambako alikuwa anacheza chini ya  kocha mkongwe Raff Rangnick, Marco Rose aliisaidia Mainz kupanda daraja hadi BundesLiga mwaka 2002 hivyo kumlazimu Klopp kumpa mkataba wa kudumu klabuni hapo.

Wakati huo Rose alikuwa beki, na alicheza kwa muda mrefu hadi mwaka 2010 alipoamua kutundika daruga. Mara baada ya kuachana na kandanda alichaguliwa kuwa kocha msaidizi klabuni hapo Mainz. 

Tangu wakati huo alifanya kazi kwa jitihada na kupanda ngazi hadi kuwa kocha mkuu. Baadaye akateuliwa kuwa kocha wa Lokomotive Leipzig ambako aliwasaidia kuepuka zahama ya kushuka daraja. Hata hivyo baada ya msimu mmja tu alishuhudia simu kutoka kwa Reb Bull Salzburg ikihitaji huduma yake kama kocha wa vijana wa kikosi chao.

Ili kupata mafanikio Marco Rose aliongoza kikosi cha chini ya miaka 16 huku akitumia mbinu za gwiji wa mfumo wa Gegenpressing Rangnick kusuka kikosi chake kipya Austria, na kuanzia hapo mipango ya maendeleo ilisukwa ili kuleta mafanikio klabuni.

Rose na Salzburg walianza kuona mafanikio kupitia kikosi chao cha vijana baada ya kutwaa ubingwa wa UEFA Youth League mwaka 2017 baada ya kuifunga Manchester City waliokuwa na mastaa vijana kama vile Brahim Diaz na Jadin Sancho, pamoja na kuwatnadika Atletico Madrid na Barcelona wakati huo.

Kuanzia wakati huo uongozi wa Salzburg uliamua kumkabidhi jukumu la kuinoa timu ya wakubwa, ambako alishinda mechi 37 kati ya 50 za Ligi Kuu ya Austria.

Na zaidi Red Bull ilisonga mbele na kufika nusu fainali ya Europa League baada ya kuitoa Dortmund katika hatua za mtoano. Ushindi dhidi ya Dortmund uliibua mshtuko na kumpa sifa nyingi Marco Rose. 

Sasa, baada ya kushinda kombe la Ligi na Ligi ilionekana ni vigumu Red Bull Salzburg kumzuia Marco Rose kuondoka klabuni hapo, huku Klopp akiwa ameshatabiri namna mwalimu huyo anavyoweza kufanya vizuri Dortmund. 

“Namwamini kwa kila kitu. Marco anaweza kufanya kazi katika klabu yoyote, anafanya kazi kisasa na mbinu za wakati huu, nan i kocha wa aina yake,” Ilikuwa kauli ya Jurgen Klopp wakati akihojiwa na vyombo vya habari mwaka 2019. 

Uwezo wa Marco Rose kufundisha kandanda ni mkubwa na hilo halipingiki kabisa. kwahiyo klabu kama Gladbach ilipokuja kumpa ofa hailikuwa suala la kufikiri mara mbili tena. Kilichoshangaza pekee wakati anaajiriwa Gladbach ilikuwa anachukua nafasi ya Dieter Hecking, ambaye aliongoza klabu hiyo kushika nafasi ya tano ya Bundesliga.

Hata hivyo mkurugenzi wa michezo wa Gladbach, Max Eberl hakutaka kukosa nafasi ya kumwajiri Marco Rose klauni kwao, kwa sababu klabu za Hoffeinheim, Schalke na Wolfsburg zote zilimtupia ndoano ya kujiunga nao.

“Huwa tunachunguza makocha wetu kubaini vipawa vyao, na miongoni mwao alikuwa Marco Rose hivyo isingekuwa rahisi kungojea zaidi. nikiwa mkurugenzi wa ufundi kupata nafasi hiyo ya kumwajiri niliona ni moja tu, hakuna zaidi. Pengine ni suala la asilimia 90, unachagua iliyopo sokoni ambayo itakuwa kitu kinachokufaa ili kupata suluhisho la kitu unachotaka.”

“Marco alikuwa sokoni na hakukataa ofa yetu, labhda lilikuwa jambo la kawaida kwa  Dieter Hecking kuendelea kuinoa klabu yetu, lakini tulihitaji kitu zaidi na hicho kilikuwa kwa Marco Rose.

Naye Rose hakuonekana kuwaangusha wale waliogundua uwezo wake katika soka, kwani alifanikiwa kuipaisha Gladbach hadi hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Ulaya na kupangwa na timu za Real Madrid, Inter Milan na Shakhtar Donesk. 

Ingawa habari za kuondka Marco Rose kwenda Dortmund zitawakera mashabiki wa Gladbach lakini ukweli ni kwamba Iduna Park inahitaji bingwa wa mbinu za mchezo ili kuibuka na ushindi pamoja na kuleta mafanikio. Ingawa Marco mwenye umri wa miaka 44 hajaanza kazi Dortmund lakini mashabiki wa Iduna Park wameanza njozi za mataji kama zama za Jurgen Klopp.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version