Menu
in , , ,

Blatter kung’oka Fifa

Mbuyu unang’oka. Ndivyo unavyoweza kuelezea uamuzi wa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter kuamua kuachia ngazi baada ya kuzongwa na tuhuma nyingi za rushwa.

Blatter (79) ametangaza uamuzi wa kujiuzulu uongozi huo kwa maelezo kwamba haoni akiungwa mkono na ulimwengu wa soka, lakini zikiwa ni siku nne tu tangu achaguliwe tena kuwa rais kwa muhula wa tano.

Fifa

Alitakiwa siku nyingi kutogombea tena na baadaya wajumbe saba waandamizi wa Fifa kukamatwa na mamlaka za Uswisi jijini Zurich kwa maombi ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), aliendelea na uchaguzi na mashirikisho husika ya soka yakampa uongozi.

Blatter amesema kwamba ataitisha mkutano mkuu maalumu wa Fifa kwa ajili ya kuchagua rais mwingine mapema iwezekanavyo, uamuzi huo ukija wakati Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) likitafakari hatua za kuchukua ili kutompa ushirikiano Blatter.

Michel Platini, Rais wa Uefa aliyejiita kuwa rafiki wa Blatter alimshauri ang’atuke siku chache kabla ya uchaguzi, akimrejea kama rafiki aliye matatani, lakini Blatter akamjibu kwamba alichelewa mno kumpa wazo hilo.

“Naona kwamba uongozi wangu hauungwi mkono na kila mmoja. Mkutano wa kawaida wa Fifa utafanyika Mei 13, 2016 lakini hadi huko ni mbali kwa hiyo nitaitaka kamati ya utendaji kuandaa mkutano maalumu wa uchaguzi wa mrithi wangu mapema iwezekanavyo,” akasema Blatter.

Mkongwe huyo ambaye ni raia wa Uswisi aliyekaa madarakani kwa miaka 16 anasema kwamba lazima muda wa kutosha utolewe kwa ajili ya wagombea wazuri zaidi kujitokeza na kufanya kampeni.

Blatter alimshinda mwana wa mfalme wa Jordan, Ali bin al-Hussein kwenye uchaguzi wa wiki jana baada ya wagombea wengine kujitoa. Hata hivyo ushindi wake ulilalamikiwa na wengi waliokuwa wakisema kwamba soka itaingia kwenye matatizo kutokana na harufu ya rushwa.

Wakati Marekani wameshaanza uchunguzi na wanatarajia kuwashitaki maofisa wa Fifa wakihusishwa na rushwa na utakatishaji wa fedha chafu, Uswisi wamefungua jalada kwa ajili ya kuchunguza masuala ya mchakato wa uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 Urusi na 2022 Qatar.

Tayari kuna matarajio kwa baadhi ya wadau kwamba huenda uenyeji wa Qatar utafutwa, ikizingatiwa kwamba kuna madai ya kutolewa rushwa kwa wajumbe kadhaa, wakiwamo wa Afrika. Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), Issa Hayatou anadaiwa kupewa hisani na bara hilo ni moja ya yaliyotoa uungwaji mkono kwa Blatter.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version