*Rais wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Sepp Blatter amesema mchezaji wa AC Milan,
*Kevin-Prince Boateng amefikisha ujumbe kwa kuvunja mechi baada ya kutukanwa.
Akizungumza mjini Zurich, Blatter amesema katika soka hakutakiwi kuwapo ubaguzi na kwamba Fifa haina suluhu ya aina yoyote dhidi ya wabaguzi.
Pamoja na kusema kwamba hilo si suluhisho la kudumu, kwa vile wadau wanatakiwa kuifuata mizizi ya ubaguzi ilipo na kuing’oa, Blatter amesema Boateng ameonesha ujasiri mkubwa.
Kilichotokea ni kwa Boateng kuchukua mpira, kuupiga jukwaani kwa mashabiki wa timu ya Pro Patria walikokuwa wakimtolea ishara za ubaguzi za nyani, kisha akatoka uwanjani akifuatwa na wachezaji wa Milan.
Ilikuwa mechi ya kirafiki, lakini Boateng ambaye ni raia wa Ghana, anasema hata ikiwa kwenye ligi ya taifa au mashindano ya kimataifa, atatoka uwanjani.
Kitendo cha Boateng kimezua mjadala mzito miongoni mwa wadau wa soka, ambapo baadhi ya wachezaji wa sasa na wa zamani wanamuunga mkono.
Baadhi ya wanaoungana na Boateng ni ofisa wa Manchester City, Patrice Vieira; Rio Ferdinand wa Manchester United na nahodha wa City, Vincent Kompany.
Boateng amepata kuchezea timu za Uingereza za
Portsmouth na Tottenham Hotspurs.
Blatter anasema Fifa haitakuwa na uvumilivu katika kukabiliana na wanaoendekeza ubaguzi.
Blatter anasema wachezaji wanapochukua hatua ya kutoka uwanjani, maana yake ni kwamba timu huvunja mechi, hivyo washabiki wanaobagua kukosa wa kuwaagua.
“Kitendo kile kilifikisha ujumbe hasa, kwamba washabiki wanatakiwa wajiheshimu, kwa sababu mchezaji alikimbia na wengine wakamfuata na baada ya hapo hakuna mtazamaji ambaye angeweza kuendelea kudhalilisha,” anasema Blatter.
Boateng kwa upande wake, katika mahojiano zaidi baada ya siku ile, anasema kwamba huo ni ujumbe wake kwa Fifa kwamba wanatakiwa kuamka na kuchukua hatua kali.