Bingwa mpya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu mpya wa mwaka 2012/2013 anatarajiwa kupata zawadi ya Sh. milioni 70, imefahamika.
Mshindi wa ligi mbali na zawadi hiyo kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya huduma za simu ya Vodacom, atapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.
Chanzo kimeieleza NIPASHE kuwa mshindi wa pili ambaye huiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho, atapata zawadi ya Sh. milioni 50, wakati mshindi wa tatu atapewa Sh. milioni 30.
“Jana (juzi) ndio tumewarudishia rasimu ya mkataba na kipengele cha zawadi kimetengewa Sh. milioni 150,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongezakuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndio wasimamizi wa mchezo huo nchini watasaini mkataba wa miaka mitatu na kwa msimu huu Vodacom itatumia kiasi cha Sh. bilioni 1.7.
Kiliongeza chanzo hicho kuwa katika mkataba huo wamezingatia mambo mbalimbali ikiwamo gharama za nauli za timu kutoka kituo kimoja hadi kingine, ongezeko la zawadi na posho za waamuzi ambazo awali hazikuwa zikilipwa na mdhamini huyo.
“Kiasi cha udhamini kitakuwa kinaongezeka kwa kila msimu kutokana na kuzingatia gharama halisi za uendeshaji,” kiliongeza chanzo chetu.
Kiliongeza chanzo hicho kuwa huenda klabu zikapata jezi mapema ama zikachelewa kutokana na zoezi hilo la kusaini mkataba mpya kutokamilika kwa wakati.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema jana katika taarifa yake kwamba Vodacom watasainiwa mkataba huo mpya Jumanne ya Septemba 11 mwaka huu kwenye ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Wambura hakuwa tayari kusema lolote lililomo kwenye mkataba huo mpya.
Simba ndio bingwa mtetezi ambaye alipata zawadi ya Sh. milioni 40. Mshindi wa pili wa msimu uliopita alikuwa akipata Sh. milioni 30 na wa tatu Sh. milioni 20.
Klabu za Simba na Yanga zina wadhamini wengine ambao ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inayowapatia jezi na vifaa mbalimbali vya michezo mara mbili kwa msimu.
Ligi Kuu ya Bara itaanza Septemba 15 lakini itazinduliwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaofanyika Jumanne kwa kuwakutanisha Simba na mshindi wa pili wa msimu uliopita, Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.