Menu
in

Bila fedha Ligi zetu zitakuwa nyanya

Tanzania Sports

Michezo na burudani itapiga hatua ikiwa kutakuwa na uwezekaji wa fedha,vipaji na mipango madhubuti. Bila kuwa na fedha za kutosha mchezo wa soka utasota na kusubiri mafanikio kwa miaka hata 100 ijayo. Kwanini nasema kwa hitimisho hilo? 

Fuatana nami katika makala haya kuona mifano inayodhihirisha bila fedha ligi yetu itabaki kuwa nyanya yaani laini,isiyo na ushindani,mvuto na itabaki kuwa na viongozi na wachezaji wa zimamoto.

Mosi, hivi karibuni wapenzi wa soka walishuhudia wawakilishi wa Tanzania klabu ya Biashara United wakishindwa kusafiri kwenda nchini Libya kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Ahly Tripoli. Biashara United ilishindwa kwenda huko ikiwa na mtaji wa mabao mawili mkononi baada ya mchezo wa kwanza. 

Tukio la Biashara United kuomba kuahirishwa mechi yake siku moja kabla halikuhitaji akili kuwapotezea. Ndiyo, hata ningelikuwa mimi ndiye bosi wa Shirikisho la soka Afrika CAF, nsingewasikiliza Biashara United kwakuwa hakukuwa na sababu zenye ushawishi za kuahirisha mechi yao. 

Lakini kubwa zaidi Biashara United walishindwa kwa sababu hawakuwa na fedha. Duru za kimichezo zimemwambia mwandishi wa makala haya kuwa uongozi wa Biashara United ilikimbilia kununua tiketi katika ndege za kampuni ndogo ambazo hazina uhakika wa safari. 

Hivyo hata ndege yao ilipokatishwa safari wakajikuta hawana mpango wa pili wa kwenda Libya. Duru hizo zinasema laiti wangelikuwa wamekata tketi kwa mashirika makubwa kama Emirates bila shaka wangewezeshwa namna ya kwenda Libya. 

Pili, tukio lingine linahusu timu ya Arusha Fc ambayo ilizuiliwa kutoka katika nyumba ya wageni waliyofikia kwa sababu ya kudaiwa shilingi milioni 1.8. deni hilo lilisababisha uongozi wa nyumba ya wageni waliyofikia timu hiyo kuwazuia kutumia na kuondoka hali ambayo ilisababisha wachezaji kuketi na kulala kwenye gari lao walilokuja nalo. 

Hali ya fedha ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili. Mwenendo wa timu hiyo kwa sasa ni kuomba michango ya hali na mali kwa wadau wa soka ili waichangie iendelee kuhudumu katika mchezo wa soka.

Tatu, ushindani katika Ligi yetu ingawa umeongezeka lakini bado inaonekana Yanga,Simba na Azam zitabaki kuwa kubwa zaidi kuliko zingine 13. Kuwa na ushindani katyika Ligi ni njia mojawapo ya kusaidia wachezaji,viongozi na wadau wa soka kufurahia mchezo wenyewe na kuibua vipaji zaidi. 

Nne, kumekuwa na mashambulizi katika mitandao mbalimbali nchini kwa wadhamini wanaodhamini timu zaidi ya moja. Chuku mfano kampuni ya GSM inawadhamini Namungo,Coastal Union na Yanga. Vilevile kampuni ya Sportpesa inwadhamini Namungo,Yanga na Simba. 

Udhamini huo una maana kuwa timu zinapokea fedha na kutangaza majina ya wadhamini wao. Mashambulizi yanayoelekezwa kwa wadhamini yanajenga hoja kuwa hakuna ushindani wa haki pale mdhamini mmoja anapozidhamini zaidi ya timu moja. 

Hii unaeeza kusema kwamba Sportpesa kuidhamini Yanga,Simba na Namungo ni kama vile hakuna ushindani wake. Vilevile udhamini wa GSM ni kama hanazuia ushindani wa haki. Hoja hizi zote naweza kuzitafsiri kuwa zinalenga kutaka uwazi katika mikataba ya wadhamini tu. 

Kinyume cha hapo, ikiwa kuna hila zozote maana yake tunajaribu uwakatisha tamaa na kuwafukuza wadhamini ambao fedha zao zinahitajika katika mchezo wa soka. kwa mataifa yaliyopiga hatua kisoka kama England, kampuni yaCazoo inadhamini Eveton na Aston Villa kwa wakati mmoja. 

Je unaweza kusema hakuna ushindani wa haki EPL kiasa tu kampuni moja? Kwamba Cazoo, Sportpesa,GSM zinaweza kuchochea maamuzi ya kupindisha sheria ili kuibeba timu fulani? Ni kwanini Yanga wanaodhaminiwa na Sportpesa hawakutoboa kimataifa kama walivyo wezao Simba? 

Je kulikuwa na ukosefu wa ushindani wa haki huko uliowaondoa Yanga? Na msimu uliopita Yanga walichapwa 1-0 na Coastl Union ambao walifungwa 7-1 na Simba, Union na Yang azote zinadhaminiwa na GSM. Kama sio fedha za GSM kuwekeza katika mchezo wa soka, tunaongelea haki ya ushindani katika upande mmoja huku upande wa pili ulio chanya hazungumzii. 

Ikiwa leo taifa linashuhudia aibu ya wawakilishi wao kushindwa kwenda kucheza mchezo wa marudiano Libya kwa sababu ya ukosefu wa fedha, je tunatafuta haki ya ushindani kwa kujenga hoja za upande mmoja pasipo maumuisho? 

Ni kwanini tuone ushindani wa haki katika sura ya kampuni fulani kudhamini timu badala ya matatizona matundu yaliyoko katika timu zetu? je tunataka tena akina Harmonize wajitokeze kuokoa jahazi dakika za majeruhi kwa kulipia nauli na chakula kama alivyowahi kufanya kwa Ndanda? Je njia hiyo itakuza soka letu?

Hivi leo tunashuhudia timu inazuiliwa kwenye nyumba ya wageni kwa sababu ya kukosa fedha ndogo tu, lakini hatupo tayari kuwasaidia hawa wapate wadhamini kama GSM, Sportpesa, Cazoo na wengine ili kuondokana na aibu za kuzuiliwa hotelini na kulala kwenye magari? 

Katikati ya dhiki ya fedha tunaweza kuwasajili wachezaji wa kimataifa wenye maarifa ya kuchangamsha Ligi yetu? Namna gani tunaweza kuwashawishi wadhamini waje kwenye soka zaidi ikiwa longolongo zitakuwa ndio msingi wa kuendesha soka. Ni namna gani tunaifanya timu zetu ziwe na uwezo wa kupiga hatua zaidi kuliko kuwashambulia wale wanaowekeza fedha huko?

Kama nilivyosema katika aya ya kwanza, Ligi yetu itakuwa nyanya kama hakuna fedha. Ligi isiyo na fedha haivutii kampuni kudhamini wala kuwekeza. 

Ligi isiyoeleweka haivutii wachezaji wan je kuja kucheza, badala yake ikiwa kuna uwekezaji kupitia kampuni zinazodhamini ndizo zitaibua ushindani na maarifa ya wachezaji wengine pamoja na kunufaisha wadau mbalimbali wa mchezo wenyewe. Bila fedha Ligi yetu itadumaa.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version