Menu
in , , ,

BERNABEU ILISIMAMA, LEO DUNIA IMEINAMISHA KICHWA

Tanzania Sports

Hakuna kitu kigumu kama kucheza katika uwanja wa Santiago Bernabeu.

Uwanja ambao wachezaji nguli washapita pale na kuweka rekodi nyingi za
soka duniani.

Uwanja ambao una mataji mengi ya kombe la klabu bingwa barani ulaya.

Kombe ambalo lina ushindani mkubwa lakini wao ndiyo Wafalme kwa kulichukua.

Wao ndiyo waliochukua mara nyingi zaidi, ikiwa ni mara 12 kuzidi timu
yoyote barani ulaya.

Huu ni ubabe ambao anao Real Madrid.

Atajivunia, ataringa ,atakudharau na wakati mwingine atakutukana kwa
sababu anajua yeye ndiye bingwa wa historia wa klabu bingwa barani
ulaya.

Jeuri hiyo anayo, hata jeuri ya pesa anayo na hapo bado hujamgusa
katika Ligi kuu ƴya Hispania ( La Liga).

Ambapo ndiye anayeongoza kwa kuchukua mara nyingi akiwa amechukua mara 33.

Akiwa ndiye mtu mwenye mafanikio makubwa katika timu za Hispania.

Mafanikio ambayo yameifanya kuwa timu kubwa duniani.

Mafanikio ambayo yamewapa jeuri ya pesa na hata mashabiki wake wana
jeuri kweli kweli.

Wao ndiyo wanaamini ni mashabiki bora wa klabu bora duniani.

Wanaamini mchezaji bora duniani lazima apitie katika timu yao ndiyo
maana wakajiita Galactico.

Hizi ndizo jeuri za Real Madrid, jeuri ambazo huufanya uwanja wa
Santiago Bernabeu kuwa mgumu kwa mpinzani anayekuja pale.

Mpinzani akikanyaga nyasi za uwanja huu mchezaji wa kwanza kushindana
naye ni shabiki wa Real Madrid.

Hawa ni wagumu kukubali kuwa wamezidiwa ubora na mpinzani.

Huwezi kuwaaminisha kawaida na wakakuamini, labda ufanye kazi ya ziada.

Kama kazi ambayo aliifanya Ronaldinho Gaucho tarehe 19/11/2005 katika
usiku wa kihistoria wa El Clasico.

Usiku ambao Ronaldinho Gaucho alikuwa katika kiwango cha mwezini.

Mbalamwezi iliwaka katika utosi wa kiwango chake.

Alifanya kazi iliyokuwa inaonekana ngumu kuwa nyepesi.

Kiasi kwamba uwanja mzima wa Santiago Bernabeu ulisimama na
kumshangilia kwa kiwango alichokionesha.

Kila shabiki kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu alisimama na
kukishujudia kiwango cha Ronaldino Gaucho.

Haijalishi Real Madrid kupoteza mchezo ule, lakini walishukuru na
kumpongeza kwa burudani ambayo walipewa na Ronaldinho Gaucho.

Kwa mara ya kwanza mashabiki wa Real Madrid walipokea kipigo kitamu.

Kipigo kisichoumiza, kipigo ambacho waweza kupigwa na ukatamani
kuendelea kupigwa na hii ni kwa sababu ya Ronaldinho Gaucho.

Mchezaji ambaye kila mtu aliyekuwa akimshuhudia uwanjani alikuwa
anabubujikwa na machozi ya furaha kwa kutazama kiwango chake.

Wengi walikuwa wanazirudisha sifa na shukurani kwa mwenyezi Mungu kwa
kuwezeshwa kumuona Gaucho.

Mtu ambaye alikuwa na sanaa tamu za mpira, sanaa ambazo zilianzia
kwake na zikaishia kwake.

Hatujapata tena mtu mwenye sanaa kubwa kama yake.

Mpaka muda huu ameshatangaza kustaafu kucheza soka.

Hatutomuona tena akicheza soka la ushindani.

Mara ya mwisho kwake yeye kucheza soka la ushindani ilikuwa mwaka 2015
akiwa na klabu ya Fluminense.

Hatukuwahi kumuona tena akicheza mchezo wa ushindani, wengi walidai
ameshastaafu tayari lakini tamko rasmi limetoka kuwa amestaafu.

Mshindi wa mchezaji bora wa dunia wa FIFA mara mbili 2005 na mwaka 2006.

Miaka hii ndiyo ilikuwa miaka yenye mafanikio kwake , pamoja na
kuiwezesha timu yake ya Barcelona kushinda taji la klabu bingwa barani
ulaya mwaka 2006 pia alichukua tunzo ya Ballon D’or mwaka huo wa 2006.

Nyota yake ilianza kuonekana akiwa na timu ya vijana ya chini ya umri
wa miaka 17.

Ambapo walifanikiwa kuchukua kombe la dunia la vijana la chini ya umri
wa miaka 17.

Kila mtu alikitabiria kipaji chake, hakuna ambaye aliacha kusifia kila
Gaucho alipokuwa anakanyaga mpira.

Na kuna muda mwingine waweza tamani kila muda Gaucho apewe mpira kwa
sababu alikuwa anautendea haki mpira.

Mpira ulikuwa umezaliwa kwake, na yeye alizaliwa na mpira, hakukuwa na
shaka kusema Gaucho na mpira walikuwa mapacha wa damu.

Walipendana kwa sababu kila mmoja alimpa upendo mwenzake, Gaucho
aliupa upendo mpira, na mpira ulimpa upendo Gaucho.

Kilichokuwa ƙkinabaki ni sisi kufurahia burudani ambayo ilikuwa haikinaishi.

Burudani ambayo ilikuwa na matumizi machache ya nguvu huku sanaa,
akili , ubunifu ukitawala kwenye miguu ya Gaucho.

Ndiyo maana Gaucho alikuwa hapotezi tabasamu lake kila alipokuwa
anaukamata mpira, hakuhitaji nguvu nyingi mpaka mishipa imsimame.

Kwake yeye mpira ulikuwa furaha na burudani ndiyo maana alifanikiwa
kuzikonga nyoyo zetu.

Kama umri ungekuwa na mabadilishano, ningempa Gaucho umri wake na mimi
nichukue umri wangu ili mradi tu arudi uwanjani kufurahisha wanadamu.

Lakini ndivyo haiwezekani, na ameshatuaga tayari, vichwa vyetu
tumeviinamisha kwa majonzi, tunatamani arudi tena ila wakati ni ukuta
na mwisho wake wa kulitumikia soka umeshafika na hakuna budi iwe hivo
ili kuruhusu kizazi ƙkingine.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version