Menu
in , ,

Benitez bosi mpya Real Madrid

Kocha wa zamani wa Liverpool, Chelsea na Napoli, Rafa Benitez ametangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa Real Madrid.

Benitez anachukua nafasi ya Mtaliano, Carlo Ancelotti aliyefutwa kazi majuzi baada ya kumaliza msimu bila taji lolote, licha ya mwaka jana kuwapatia ubingwa wa Ulaya, ikiwa ni mara ya 10 kwa timu hiyo kuutwaa.

Benitez alitangaza kuondoka Napoli hivi karibuni, na mwenyewe akiwa ni raia wa Hispania aliyepata kueleza ndoto yake ya kufanya kazi Santiago bernabeu, alisababisha wengi kuanzisha tetesi kwamba atajiunga huko.

Benitez anakuwa kocha wa nane katika kipindi cha miaka 10 na wa 12 tangu kuanza kwa karne hii atakuwa na kazi ya kurejesha heshima kwa Madrid, na ameingia mkataba wa miaka mitatu hapo.

Makocha wengine waliopata kufukuzwa ni pamoja na wenye majina makubwa, kama Jose Mourinho na Fabio Capello licha ya kuwapatia mafanikio klabu hiyo kubwa barani Ulaya. Benitez amezaliwa Madrid, kama ilivyo kwa kipa wa Manchester United, David De Gea anayesemwa kwamba atajiunga Madrid kiangazi hiki.

Hata hivyo, katika mazungumzo yake na wanahabari, Benitez amesema kwamba anapenda aina ya soka anayocheza mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling na kuzidi kutia wazo kwamba chipukizi huyo aliyekataa mkataba mpya Anfield atamfuata Benitez.

Benitez aliwafundisha Napoli kwa miaka miwili na sasa ameahidi kwamba ataileta soka ya kiwango cha juu Bernabeu pamoja na makombe.

Barcelona wameibuka kuwa na mafanikio zaidi msimu huu nchini Hispania, baada ya kutwaa ubingwa wakiwapita Madrid na pia wakatwaa Kombe la Mfalme. Hivi sasa wanasubiri kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Juventus wikiendi hii.

Benitez alizaliwa Aprili 16, 1960 na amepata kucheza soka katika academia ya Real Madrid katika muda wake mwingi wa ujana. Alichanganya soka pamoja na masomo ya chuo kikuu akiwa katika ligi ya madaraja ya chini nchini Hispania.

Alijiunga kwenye benchi la ufundi la Real Madrid akiwa na umri wa miaka 26, na amepata kuwa kocha wa kikosi cha pili na kile cha vijana chini ya umri wa miaka 19 kabla ya kuwa kocha msaidizi wa timu ya wakubwa.

Aliondoka na kufanya kazi kwa muda mfupi na bila mafanikio kwenye klabu za Real Valladolid na Osasuna . Klabu nyingine alizofundisha kati ya 1997 na mwaka huu ni Extremadura, Tenerife, Valencia, Liverpool, Inter Milan, Chelsea akiwa kocha wa muda kabla ya kwenda Napoli.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version