KATIKATI ya huzuni ya maelfu ya watanzania wamejikuta wakilazimika kulia kwa furaha na wengine kushangilia kwa nguvu zote. Kutoka huzuni ya kuwapoteza raia 20 kutokana na kuporomoka ghorofa moja katika mtaa wa Congo na Mchikichi jijini Dar Es Salaam hadi kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON mwaka 2025 nchini Morocco. Bado shamrashamra zinaendelea katika mioyo ya watanzania kutokana na furaha ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Guinea wa Taifa Stars. Ushindi huo umemfanya winga machachari wa Taifa Stars, Simon Msuva kubakiza bao moja tu kufikia rekodi ya nyota wa zamani Mrisho Khalfan Ngassa. Simon Msuva amepachika bao lake la 24 kwa Taifa Stars ikiwa moja pungufu dhidi ya Ngassa mwenye mabao 25. Katika safari ya kufuzu mashindano hayo makubwa barani Afrika TANZANIASPORTS inakuangazia makosa matatu ya benchi ya ufundi katika safari ya kufuzu AFCON.
Matamanio dhidi ya uwezo
Benchi la ufundi linaongozwa na kocha Hemed Morocco akiwa na makocha wazawa Juma Mgunda, Jamhuri Kihwelo na Amri Kiemba pamoja na timu ya madaktari. Katika safari ya kufuzu AFCON benchi la ufundi lilifanya kosa ambalo walirekebisha baadaye kwa kuwaita wachezaji wengi vijana ili kupigania mechi zilizobaki za kufuzu. Kaimu kocha mkuu, Hemed Morocco alitamani vijana wengi walioitwa Taifa Stars wamnletee matokeo mazuri na kufanikisha safari ya kufuzu.
Katika kikosi chake aliwatema Dickson Job, Mbwana Samatta, Simon Msuva na nyota wengine wenye uzoefu. Kikosi chake kilipocheza dhidi ya Ethiopia kilikosa kumaliza mechi katika mchezo wa kwanza kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Kushindwa kuumaliza mchezo ule kwa kuwafunga Ethiopia jijini Dar Es Salamaa kulifanya safari ya kufuzu mashindano hayo iwe ngumu. Benchi la ufundi lilifanya kosa hili na kocha Hemd Morocco hajatamka kuomba radhi kwa maneno badala yake amefanya kwa vitendo kwa kuwaita nyota hao katika safari yake ya kufuzu.
Kimsingi matamanio ya kocha hayakuendana na uwezo wa rasilimali alizokuwanazo. Hivyo alihitaji uzoefu wa Mbwana Samatta na Simon Msuva. Kiufundi Mbwana Samatta amewaacha mbali sana kiweledi,ujuzi,uwezo na uzoefu kwahiyo ilihitajika nguvu zake pamoja na Simon Msuva kuimarisha kikosi chake.
Kutibua Kombinesheni ya safu ya ulinzi
Akizungumzia uamuzi wa kumwacha nje ya kikosi chake beki mahiri Dickson Job kaimu kocha Hemed Morocco alisema kwamba nyota huyo hastahili kucheza nafasi ya beki wa kati. Kocha huyo alieleza kuwa sababu ya kumweka kando ilikuwa ni kimo chake kutotosheleza kucheza nafasi hiyo. Kiufundi hadi sasa na kwa timu zote za Ligi Kuu hakuna kombinesheni inayofanya kazi kubwa na kuipaisha klabu yao kama ya Dickson Job na Ibrahim Bacca. Pamoja na matamanio ya kocha huyo kumwita nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto bado kulikuwa na pengo la kombinesheni.
Kila idara kwenye mpira wa miguu kunakuwa na kombinenga fulani ya wachezjai ambao ushirikiano wao unatengeneza ugumu kwenye safu ya ulinzi au kufumania nyavu mara nyingi. Kuna washambuliaji ambao wanaelewana kiucheza kiasi kwamba makocha wanalazimika kuwatumia.
Wakati kocha Hemed Morocco alilaumua kimo, mwenzake aliyekuwa kocha wa Yanga Miguel Gamondi alikuwa ananufaika sana na umahiri wa kombinesheni ya Ibrahim Bacca na Dickson Job. Kwahiyo kombinesheni aliyotaka Hemed Morocco ya Ibrahim Bacca na Bakari Nondo Mwamnyeto haikuweza kufanya kazi. Imewachukua muda mrefu klabu ya Simba kumpata Ibrahim Hamza ambaye ametengeneza kombinesheni kali na Che Marlone. Simba wanajivunia safu hii hadi sasa na imewaletea matunda.
Kosa alilofanya kocha wetu ni lilile ambao lilijitokeza kwenye Ligi Kuu England (EPL) ambapo beki wa Manchester United. Lisandro Mrtinez naye alikuwa akibezwa kwa kimo kifupi. Lakini Lisandro Mrtinez ni miongoni mwa mabeki wakali wa EPL kwa sababu ya umahiri na maarifa aliyonayo. Bahati nzuri Dickson Job anao uwezo wa kucheza beki wa kati, kulia,kushoto na kiungo mkabaji ambako alipangwa mara kadhaa. Kocha Hemed Morocco alitakiwa kujisikia fahari kuwa na mchezaji mwenye uwezo wa kumpanga sehemu tofauti kama ambavyo unawez akumtumia Novatus Dismas Miroshi kama beki wa kushoto, winga wa kushoto, beki wa kati na kiungo mkabaji. Ndivyo makocha walivyo makocha na faida kubwa kuw ana mchezaji wa aina hiyo.
Eneo la golikipa
Ni dhahiri mabadiliko katika timu ni kawaida. Wachezaji wanazidiana uwezo kwahiyo Ali Salim anazidiwa uwezo na makipa wengi akiwemo Metacha Mnata. Uamuzi wa kuamini kuwa Ali Salim angeweza kulivusha Taifa ulikuwa mzigo mkubwa asioweza kuubeba. Kulikuwa na kila sababu za kuepukana na kosa hili kwa sababu ambazo hata TANZANIASPORTS imeeleza kwa kina kwa kuchambua uimara na udhaifu wa kipa wetu Ali Salim kwa nia ya kumjengea uwezo zaidi.
Eneo la golikipa tunao wachezaji ambao wanacheza vema Ligi Kuu na nje. Huenda hatujafaidi uwezo wa Kwesi Kawawa kwa sababu alikuwa anakabiliwa na presha kubwa katika mchezo mkubwa na bila uzoefu wowote. Pengine sio Kwesi Kawawa tu bali wapo makipa ambao wameonesha uwezo mkubwa kulinda lango na kufanya uamuzi.
Ni sababu hiyo hata kocha wa Taifa Stars iliyocheza mechi ya kuwania kufuzu mashindano ya CHAN, Bakari Shime hakupepesa macho, aliamua kumwita Aishi Manula badala ya Ali Salim aliyekuwa akipangwa Taifa Stars ya AFCON. Ni dhahiri tunapoelekea kwenye mashindano ya AFCON nchini Morocco tunapaswa kujiandaa vema eneo la golikipa na kuwa na uhakika wa kimaamuzi kwa makipa wetu wenye uwezo na uhodari wa kufanya uamuzi wanapokuwa langoni.