.Miaka 28 bila medali ni aibu kubwa
KWA mara nyingine, Tanzania inarejea nyumbani mikono mitupu baada ya kushindwa kuambulia medali hata moja katika michezo ya Olimpiki.
Katika michezo ya 29 iliyofungwa rasmi Jumapili iliyopita huko Beijing, China, Tanzania iliwakilishwa na wanamichezo kumi, wakiwamo wanariadha wanane waliofundwa na nyota wa zamani katika mchezo huo, Juma Ikangaa.
Wawili waliobaki walikuwa waogeleaji. Hao ni Khalid Rushako na Magdalena Moshi walioshindwa mapema kabisa.
Na kete ya mwisho ilikuwa kwa mwanariadha wa mbio za Marathoni, Samson Ramadhani ambaye katika siku ya mwisho ya mashindano, yaani Jumapili alimaliza akiwa wa 55, huku Getul Bayo na Mohammed Masenduki wakishindwa kumaliza mbio hizo ambazo mshindi wake aliibuka Mkenya Samuel Kamau Wanjiru aliyetumia saa 2:06:32.
Wanamichezo wengine waliokuwa na tiketi za kuiwakilisha Tanzania ni Samuel Mwera (mita 800), Zakia Mrisho (5,000), Fabian Joseph, Dickson Marwa na Samuel Kwaan`g wa za mita 10,000.
Aibu hii nyingine kwa Tanzania imekuwa ikijirudia miaka nenda miaka rudi, licha ya Filbert Bayi Sanka na Suleiman Nyambui kuiondolea nchi mkosa na kutwaa medali kwa mara ya kwanza huko Moscow, Urusi mwaka 1980..
Kwa sasa, Bayi ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) wakati Nyambui ni Katibu wa Chama cha Riadha Tanzania (AT).
Kwa ujumla, matokeo ya Beijing yamezidi kuwakatisha tamaa Watanzania, kiasi cha kuonekekana ni nchi isiyo na mwelekeo kimichezo, licha ya kuwa na utitiri wa vipaji kutokana kila kona ya nchi yenye watu wanaokaribia milioni 40.
Nani ameilaani Tanzania katika michezo? Mbona michezo yote iliyokuwa inaitangaza Tanzania kimataifa inazidi kurudi nyuma?
Miaka iliyopita, riadha na ngumi ilikuwa michezo iliyoibeba sana Tanzania katika michezo ya kimataifa.
Nani asiyefahamu kwamba katika michezo ya Jumuia ya Madola ya waka 1974 huko Christchurch, New Zealand Bayi alivunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500?
Wakafuatia akina Nyambui, Ikangaa, Juma Mnyampanda, Nzaeli Kyomo na wengine wengi kutamba katika michuano ya kimataifa.
Katika ngumi waliwika akina Habibu `Master’ Kinyogoli, Bakari Selemani `Match Maker’ na wengine, kabla ya kuibuka kwa wanamasumbwi kutoka katika koo za Isangura na Matumla.
Lakini kote sasa inaonekana kuwa kama tunaelekea kuzimau, kwani badala ya kupata nafuu na kukua, tunazidi kuchoka na kukatisha tamaa.
Pengine ndiyo maana haikushangaza kumsikia Rais Jakaya Kikwete Alhamisi iliyopita akiliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, baada ya kuipa pumzi soka ya Tanzania kwa kuipatia kocha Mbrazil Marcio Maximo anayeonyesha mwelekeo wa kuifufua soka yetu, sasa anaachana kabisa na soka.
Aliahidi kuanza kuelekeza nguvu zake katika riadha, badala ya michezo mingine kama Kikapu unaokuja juu na hata kutoamatumaini ya Tanzania kwa na mchezaji wa kwanza katika ligi kubwa kuliko zote katika mchezo huo duniani, Ligi ya Taifa ya Kikapu ya Marekani (NBA). Huyo si mwingine bali ni Thabeet Hasheem Manka.
Itakumbukwa kwamba, kabla na Kikwee kuutwaa Urais mwaka 2005, ndiye aliyekuwa mlezi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania (BATA). Lakini badala ya kuamua kuupendelea mchezo wa kikapu, Kikwete maarufu kaa JK ameamua kupeleka nguvu zake katika riadha ambako siyo siri, kunaonekana kumeoza licha ya kuongozwa na watu waliokuwa mahiri katika mchezo huo.
Ni dhahiri kwamba, kama juhudi za Kikwete zitafanyiwa kazi haraka, Tanzania ina wezo mkubwa wa kuwa tishio kutokana na hazina ya wanamichezo, hasa riadha waliopo katika mikoa kama Arusha, Manyara na Singida.
Hawa, wana tofauti ndogo sana za kiufundi ikilinganishwa na wenzao wa Kenya, Sudan hata na Ethiopia ambao kila kukicha wanatikisa katika michezo mbalimbali. Tumeshuhudia Mkenya akiibuka na medali ya dhahabu katika Marathon huko Beijing.
Labda kwa `ndumba’ ya Kikwete ya kuamua kuajiri kocha mahiri wa riadha, Tanzania inaweza kuondokana na unyonge katika michezo ya kimataifa, ikiwamo Olimpiki tukianzia na mwaka 2012 huko London, Uingereza.
Hakuna shaka kwamba, haya ndiyo matarajio ya Watanzania wengi, hivyo ni jambo la kusubiri na kuona.