Mabingwa wateule wa Ujerumani, Bayern Munich wamepoteza mechi ya kwanza ya ligi, baada ya kuweka rekodi ya kushinda mechi 53.
Bayern waliotetea ubingwa huo hivi karibuni, walikuwa hawajapata kupoteza mechi ya ligi kwa idadi hiyo ya michezo tangu msimu uliopita, lakini wamekuja kujikwaa ugenini kwa timu ya FC Augsburg.
Mwenendo mzuri wa Bayern msimu uliopita ulitibuliwa na Arsenal, ambapo hawakuwa wamepata kufungwa kwenye dimba la nyumbani kwao – Allianz Arena hadi The Gunners walipowapiga kwenye mzunguko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, japokuwa vijana hao wa Arsene Wenger walitolewa.
Augsburg wanaoshika nafasi ya nane kwenye Bundesliga waliwasababishia majonzi wachezaji wa Bayern, baadhi wakilia machozi kwani walitaka wamalize ligi pasipo kufungwa na hata Jumamosi hii walitawala mchezo kwa asilimia 68.
Kiboko wa Bayern alikuwa mshambuliaji Sascha Molders aliyefunga bao pekee dakika ya 31 kwa kufyatua kitu kilichompita kipa Manuel Neuer bila kuamini. Ilikuwa kama siku ya kufa nyani kwa Bayern, kwani jitihada zao za kupata mabao zikikwama kwa shuti la David Alaba kugonga mwamba, huku Mario Gotze na Thomas Muller wakishindwa kucheka na nyavu walipokuwa na fursa hiyo.
Pengine hizi ni dalili njema za kufunguliwa neema kwa Manchester United wanaokwaana na Bayern kwenye robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano hii. Katika mechi ya kwanza Old Trafford walitoka 1-1, hivyo kama United wanataka kuingia nusu fainali lazima ama washinde mechi au watoke sare ya zaidi ya bao moja.
Mara ya mwisho kwa Bayern kufungwa kwenye ligi yao ilikuwa Oktoba 2012 waliposalimu amri kwa Bayer Leverkusen ambao wamemfukuza kocha wao, Sami Hyypia kutokana na kutofanya vyema mzunguko wa pili wa Bundelsliga. Wanashika nafasi ya tano.
Kipigo hicho ni cha pili kwa Bayern msimu huu katika mashindano yote, kwani walifungwa na Borussia Dortmund kwenye Super Cup ya Ujerumani na pia walifungwa na Manchester City kwenye hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.