*Watawazwa mechi sita kabla ligi kumalizika
Bayern Munich wametawazwa mabingwa wa Ujerumani, wakiwa wamesaliwa na mechi sita mkononi.
Bayern wameweka rekodi hiyo ya aina yake na kuwavua ubingwa Borussia Dortmund Jumamosi hii, kwa kuwachapa Eintracht Frankfurt bao 1-0.
Hii ndiyo rekodi ya kwanza kwa timu katika Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga kutwaa ubingwa mapema kiasi hiki.
Huu ni ubingwa wa 23 kwa Bayern, ambao pia wanaendelea vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakienda Italia kurudiana na Juventus Jumanne, wakiwa mbele kwa mabao 2-0 waliyopata nyumbani wiki iliyopita.
Aliyevuta ubingwa mapema Bayern ni nyota wao, Bastian Schweinsteiger, aliyefunga bao pekee Jumamosi, ukiwa ni ushindi wa 24 kati ya mechi 28 msimu huu.
Bayern hawakupata kutwaa kombe kubwa tangu 2010, na hii ni zawadi kubwa kwa kocha Jupp Heynckes anayeng’atuka, na nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa kocha wa Barcelona, Joseph ‘Pep’ Guardiola.
“Hii ni timu kubwa yenye kocha wa aina yake, ni furaha kubwa kutwaa taji hili,” akasema Schweinsteiger.
Ubingwa huo umekuja licha ya Heynckes kupumzisha baadhi ya nyota wake kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano dhidi ya Wataliano.
“Si jambo la kawaida kutwaa kombe hili baada ya mechi 28 tu, ni furaha isiyo kifani. Moja ya tunu tulizoonyesha msimu huu ni kwamba hii ni timu kubwa.
“Ukubwa huu unatokana na wadau wake kuwa wana uelewano mkubwa, hivyo kwamba tuna uhakika wa kutwaa chochote katika Ligi ya Mabingwa” akasema kocha Heynckes.
Ushindi wa jana wa Borussia Dortmund – mabingwa wa misimu miwili iliyopita haukuweza kuwasaidia kurejesha ndoto za kutetea taji. Waliwafunga Augsburg mabao 4-2.
Kiungo wa Dortmund aliyetoka Liverpool Januari, Nuri Sahin, alisema hawana hiana na ubingwa kwenda Bayern na wanawapongeza kwa mafanikio yao.