Menu
in , ,

Barcelona wazuiwa kusajili


*Fifa yawapa marufuku kwa miezi 14
*Walikiuka usajili wachezaji wadogo

Mabingwa wa Hispania, Barcelona wamepata pigo kubwa baada ya kupigwa marufuku kufanya usajili kwa mwaka mmoja na miezi miwili.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limechukua uamuzi huo kutokana na Barcelona kuvunja kanuni za shirikisho hilo kwa kusajili mchezaji wa kimataifa mwenye umri chini ya miaka 18.

Kwa adhabu hiyo, sasa Barca hawataweza tena kufanya usajili wowote hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2015, ikimaanisha hawatafanya usajili majira yajayo ya joto wala dirisha dogo la Januari.

Mbali ya adhabu hiyo, Fifa limewapiga faini Barcelona kiasi cha dola 305,000. Marufuku ya kusajili ni pigo kubwa kwa Barca kwa sababu imekuwa na msimu mgumu.

Ni klabu ambayo majuzi tu kipa wake namba moja, Victor Valdes aliumia vibaya na imeelezwa kwamba atakuwa nje kwa miezi saba, ambapo Barca walishajipanga kuziba nafasi yake mwisho wa msimu, maana pia alitangaza kwamba angeondoka.

Kadhalika Nahodha Carles Puyol ambaye amekuwa akiumia mara kwa mara goti, alitangaza kukatisha mkataba wake mwisho wa msimu, akiamini hangeweza tena soka ya ushindani, ili kuiachia klabu isajili mtu wa kufaa.

Klabu hiyo iliyotwaa ubingwa wa dunia mara nne, ilikuwa imeshadhamiria kumsajili golikipa wa Borussia Monchengladbach, Marc-Andre ter Stegen na wiki iliyopita tu walikubaliana kumsajili kiungo wa kimataifa wa Croatia, Alen Halilovic.

Barcelona pia imepita kwenye magumu juu ya usajili wa nyota wake, Neymar, ikidaiwa kwamba palikuwa na ukwepaji wa kodi na kupindisha taratibu kiasi kwamba Rais wa Barcelona, Sandro Rosell alijiuzulu Januari na nafasi yake kuchukuliwa na Josep Maria Bartomeu.

Kadhalika hali hii inaiharibia Barcelona machoni pa watu waliokuwa wakiiheshimu sana, zikiwamo kampuni kubwa na mashirika yaliyojihusisha nayo, kama Unicef na Qatar Airways.

Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) nalo limeadhibiwa kwa kupigwa faini ya dola 340,000 na kuonywa kurekebisha mara moja utaratibu wake wa kuratibu mfumo uliopo wa soka, hasa kuhusu uhamisho wa wachezaji wadogo wa kimataifa. Wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya mwaka mmoja.

Kanuni za Fifa zinasema kwamba uhamisho wa kimataifa unaruhusiwa tu ikiwa mchezaji husika ana umri wa miaka zaidi ya 18, vinginevyo lazima mchezaji husika atimize moja ya vigezo vitatu vya uhamisho.

Vigezo hivyo ni kwa mchezaji kuhamia kwenye klabu ya nchi ambayo wazazi wake wamehamia ikiwa mchezaji ana umri kati ya miaka 16 -18 ana uraia tofauti nje ya Umoja wa Ulaya au eneo la kiuchumi la Ulaya. Atatakiwa kuishi ndani ya uzio wa kilometa 100 kutoka klabu ilipo.

Uchunguzi wa Fifa umegundua wachezaji kadhaa walio chini ya umri wa miaka 18 waliosajiliwa na kuchezea klabu hiyo kati ya 2009 na 2013 pasipo kutimiza vigezo hivyo.

51.577957-0.130428

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version