Menu
in , ,

Barcelona waangukia pua

*Marufuku ya kutosajili yaidhinishwa

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limetupilia mbali rufaa ya Barcelona, hivyo dirisha hili la usajili likimalizika hawaruhusiwi kusajili mchezaji yeyote hadi Januari 2016.

Barcelona walipigwa marufuku kufanya usajili kwa miezi 14 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukiuka kanuni zinazohusu usajili wa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 18.

Hata hivyo, uamuzi huo ulisitishwa baada ya Barca kupewa nafasi ya kukata rufaa, na ni wakati huo walifanikiwa kumsajili mshambuliaji Luis Suarez wa Liverpoo, beki wa kati Thomas Vermaelen wa Arsenal, na kipa Marc-André ter Stegen wa  Borussia Monchengladbach.

Kadhalika walifanya usajili wa mlinzi Jeremy Mathieu kutoka Valencia, kipa Claudio Bravo wa Real Sociedad, kipa Jordi Masip wa Barcelona B, kiungo Ivan Rakitic wa Sevilla na kiungo Rafinha aliyechukuliwa kwa mkopo kutoka Celta Vigo. Barca wametumia pauni milioni 130 kwa wachezaji wote hao.

Marufuku hiyo ya miezi 14, hata hivyo, inaanza kwenye dirisha lijalo la usajili, ndiyo maana wanaruhusiwa sasa kuendelea na usajili na katika kujiweka sawa kwa kipindi hicho kigumu, huenda watasajili wachezaji wengi zaidi msimu huu.

Taarifa ya Klabu ya Barcelona imepingana na uamuzi huo, ikasema wataendelea kupigania maslahi yao kwa kwenda kwenye mamlaka kubwa zaidi ya rufaa, yaani Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Wamedai kwamba adhabu hiyo haiitendei haki akademia yao ya La Masia, inayochukuliwa kama msingi wa mafanikio ya klabu katika miaka ya karibuni. Wachezaji hujengwa kwa falsafa ya jinsi mchezo unavyotakiwa kuchezwa na wengi wa wachezaji wa kikosi cha kwanza, wakiwamo Lionel Messi, Andres Iniesta na Xavi Hernandez wametoka kwenye akademia hiyo.

Barcelona pia wameamriwa kulipa faini ya £305,000 na kuagizwa kuweka sawa masuala yote yanayohusiana na wachezaji hao wadogo ambao majina yao hayakuwekwa hadharani. Marufuku hiyo ni kwa wachezaji wa ndani na wa kimataifa.

Shirikisho la Soka la Hispania nalo limeadhibiwa kulipa faini ya £340,000 kwa kunyamazia ukiukwaji huo, na limetakiwa kuweka mambo sawa katika mfumo uliopo wa soka juu ya taratibu za uhamisho wa wachezaji watoto wa kimataifa ndani ya mwaka mmoja.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version