Menu
in , , ,

Barcelona mabingwa Ulaya

Dhamira ilikuwa kubwa kwa Juventus kuutwaa ubingwa wa Ulaya lakini walikuwa Barcelona waliofanikiwa kuchanga vyema karata zao.

Katika mtanange mgumu uliofanyika Uwanja wa Olimpiki jijini Berlin, Ujerumani kila timu ilikuwa ikiwania kutia kimiani taji la tatu kwa msimu huu, baada ya mafanikio nchini mwao.

Barcelona wametawazwa mabingwa kwa mara ya tano sasa, ambapo licha ya imani ndogo waliyoanza nayo kwa kocha Luis Enrique, wamemaliza kwa nguvu.

Ilikuwa pia mechi ya mwisho kwa mkongwe wa Camp Nou, Xavi (35) aliyemaliza kwa kucheka, kwani anaondoka klabuni hapo kiangazi hiki kwenda Al Sadd ya Qatar.

Kwa Juventus ilikuwa masikitiko, pengine yaliyotarajiwa kutokana na historia, kwa sababu hii ni fainali ya sita ya ubingwa wa Ulaya kupoteza.

Barca wanajivunia kombe la tatu la Ulaya katika kipindi cha miaka sita, wakijidai kwa nguvu ya aina yake kwenye ushambuliaji katika Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.

Juve na Barca wote wametwaa ubingwa wa nchi zao na kombe moja juu kila moja – Kombe la Mfalme kwa Barcelona na Kombe la Italia kwa Juve msimu huu.

Barcelona walianza kana kwamba wangepata ushindi mkubwa na rahisi baada ya Ivan Rakitic kutia bao ndani ya dakika tano tu za mwanzo.

Hata hivyo, Juve waliowaondosha Real Madrid kwenye nusu fainali ya michuano hii walionesha upinzani mkali wakiwa na kipa veterani, Gianluigi Buffon aliyewakatalia Barca muda mwingi.

Walikuwa pia na mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Alvaro Morata aliyesawazisha bao kabla ya dakika ya 55. Amekuwa wa pili tu kufunga bao kwenye mechi mbili za nusu fainali na kwenye fainali yenyewe.

Wakati wa ukombozi uliwasili kwa Suarez kufunga bao baada ya Buffon kutema kiki na Messi dakika ya 68.

Ilikuwa mechi ya aina yake kwa Suarez, ikizingatiwa kwamba kwenye fainali za Kombe la Dunia, Suarez akichezea Uruguay alimng’ata mchezaji wa Juventus na Italia, Giorgio Chiellini na kupewa adhabu kali za kufungiwa na faini. Hata hivyo, Chiellini hakucheza kwenye fainali ya Jumamosi hii.

Juventus hawakuweza kufufuka tena kusawazisha na wakati mpira ukielekea ukingoni kabisa Neymar aliwaadhibu kwa kufunga bao, akisema hii ilikuwa mechi kubwa zaidi katika maisha yake. Bao lake lilitokana na kiki ya mwisho ya mechi na kipenga cha mwisho kupulizwa.

Juventus wanaweza kujiona wasio na bahati kwa kunyimwa kile walichodhani ni penati baada ya mchezaji wao, Paul Pogba kuonekana kuchezewa ndivyo sivyo na beki Dani Alves sekunde chache kabla ya Suarez kupachika bao la pili.

Hata hivyo, walikuwa na muda wa kutosha kutumia lakini hawakuwa tena na mipango thabiti kiasi cha kuwaacha Barca kuonesha soka safi bila wasiwasi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version