*Fainali ni Wajerumani Bayern na Dortmund
Haijapata kutokea, timu inayochukuliwa kuwa bora duniani, Barcelona imeondoshwa kwa aibu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutandikwa jumla ya mabao 7-0.
Maelfu ya washabiki wake walijazana Camp Nou Jumatano hii, kushuhudia kile walichokuwa wakiita kurejea kwao kwenye fomu, lakini Bayern Munich waliwanyanyua kama unyoya na kuwatupa nje.
Wakiingia Camp Nou na ushindi wa mabao 4-0 walioupata kwenye nusu fainali ya kwanza wiki iliyopita kwao, Wajerumani hao walicheza kwa kujiamini, tofauti na zinavyokuwa timu nyingine zinapofika uwanjani hapo, ambazo huishia kufungwa.
Bayern ambao kuanzia msimu ujao watakuwa chini ya kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, waliwadhibiti wapinzani wao na kufanikiwa kuwachapa mabao 3-0 na kuingia fainali na Wajerumani wenzao, Borussia Dortmund uwanjani Wembley, London, Mei 25.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu, lakini dakika tatu tu ndani ya kipindi cha pili, Arjen Robben alidokoa mpira na kuambaa nao kabla ya kuuweka sawa na guu lake la kushoto na kuzitikisa nyavu.
Barcelona waliokuwa wakihitaji ushindi wa mabao 5-0 ili wasonge mbele, sasa waliongezewa mzigo na wakati wakiutafakari, Gerrard Pique alijikuta akijifunga mwenyewe akitaka kuzuia majalo ya Franck Eibery dakika ya 72 na dakika sita tu baadaye, Thomas Muller aliongeza aibu kwa wababe hao wa dunia.
Lionel Messi alikuwa akiwatazama wenzake tu kutoka benchi alikokuwa, lakini hata angeingia huenda hapangekuwapo mabadiliko kutokana na kuwa na majeraha, kwani mechi ya awali alifunikwa kabisa, hivyo ni bora akajiuguza hadi apone.
Kocha wa Bayern, Jupp Heynckes alionekana mwenye raha, huku Tito Vilanova aliyemrithi Guardiola akiwa hana la kufanya kubadili mauaji hayo. Bayern wanaingia fainali mfululizo, kwani mwaka jana walicheza na Chelsea, wakafungwa kwa penati jijini Munich.
Hii ni mara ya kwanza kwa Barcelona kucharazwa hivi kwenye mashindano ya Ulaya, kwani rekodi inaonesha kwamba kiwango kikubwa zaidi cha kupoteza kilikuwa cha mabao yasiyozidi manne.
Walifungwa 4-0 na AC Milan 1994 kwenye fainali na pia jumla ya mabao hayo kwenye emchi dhidi ya Valencia katika Kombe la Uefa mwaka 1962 na kiasi hicho hicho cha mabao dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Real Madrid kwenye Kombe la Ulaya miaka miwili kabla.