Menu
in , , ,

Barca, Bayern safi Ulaya

Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imeanza kwa ushindi kwa
Barcelona na Bayern Munich.

Barca waliotoka kufungwa 2-1 na Real Madrid katika Ligi Kuu ya
Hispania wikiendi, walifanikiwa kuwazidi nguvu Wahispania wenzao –
Atletico Madrid kwa mabao 2-1.

Yalikuwa ni mabao ya Luis Suarez yaliyowapa nafasi kubwa mabingwa
watetezi Barca kuingia nusu fainali wakipigana dhidi ya Atletico
waliobaki watu 10 uwanjani kwenye mechi ya mkondo wa kwanza.

Atletico walitangulia kufunga bao muhimu la ugenini kupitia kwa
Fernando Torres aliyekuja kupewa kadi nyekundu hata kabla ya kipindi
cha kwanza, kwa makosa mawili yaliyoonekana kuwa ya kijinga ndani ya
dakika saba.

Barca walibadili mwelekeo wa mechi baada ya mapumziko, Suarez akifunga
bao la kusawazisha kabla ya kupiga mpira wa kichwa kwa nguvu
kuwahakikishia wenyeji ushindi.

Hata hivyo, raia huyo wa Uruguay alikuwa na bahati, kwani angeweza
kuoneshwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza, baada ya kumchezea
hovyo beki wa Atletico, Juanfran.

Timu mbili hizi zitakutana tena Jumatano ijayo kwenye dimba la Vicente
Calderon kuamua nani atasonga kwa nusu fainali.

Torres amefunga mabao 11 katika mechi 17 alizocheza kwa mashindano
yote dhidi ya Barcelona. Alianzia soka yake Atletico kabla ya kuhamia
England kuchezea Liverpool na Chelsea, lakini bao lake la Jumanne hii
linaweza kuja kuwa muhimu sana.

Alipewa kadi ya kwanza ya njano kwa kumtega mshambuliaji wa Barca,
Neymar, kabla ya kuamua pasipo sababu ya muhimu kumkwatua kwa nyuma
Sergio Busquets.

Kocha wa Atletico, Diego Simeone alionesha kukerwa na uamuzi wa
refarii wa Ujerumani, Felix Brych, ambaye pia aliwakasirisha Atletico
kwa kumpa kadi nyekundu Arda Turan kwenye mechi yao ya robo fainali
dhidi ya Real Madrid msimu uliopita.

Someone, raia wa Argentina, pia ataona kwamba hawakutendewa haki kwa
mwamuzi huyo huyo kutompa kadi nyekundu Suarez alimpomchezea rafu
Juanfran.


BAYERN USHINDI MWEMBAMBA

Arturo Vidal alifunga bao muhimu kwa Bayern Munich katika dakika ya
pili tu ya mechi dhidi ya Benfica katika robo fainali nyingine ya UCL
Jumanne hii.

Bao hilo limewapa mabingwa hao wa mara tano katika UCL ushindi muhimu,
lakini watakaotakiwa kwenda kuulinda kwenye mechi ya marudiano nchini
Ureno wiki ijayo.

Arturo Vidal akiifungia Bayern Munich dhidi ya Benfica
Arturo Vidal akiifungia Bayern Munich dhidi ya Benfica

Vidal alifunga kwa kichwa baada ya kupokea vizuri majalo ya Juan
Bernat kutoka upande wa kushoto katika shambulizi la kwanza kabisa la
mechi hiyo kwenye dimba la Allianz Arena nchini Ujerumani.

Hata hivyo, kama alivyokuwa amehofia kocha wa Bayern, Pep Guardiola,
vijana wake walikuwa na wakati mgumu kuanzia hapo na walionekana
kukabiliwa vyema na Benfica waliokuwa wamejipanga.

Nusura wageni wapate ushindi, baada ya shuti la
Jonas katika kipindi cha pili kuzuiwa na Javi Martinez.
Bayern ambao wamekuwa wakifika nusu fainali kila msimu tangu 2012
watatakiwa kujiimarisha zaidi ikiwa hawataki kuadhiriwa Jumatano ijayo
huko ugenini.

Guardiola alisema kwamba si ajabu Benfica ndiyo timu yenye ukuta mzuri
zaidi katika Ulaya yote.

Franck Ribery na Douglas Costa waliwajaribu Wareno lakini wakasimama
imara, huku mpachika mabao mahiri wa Bayern, Robert Lewandowski
akishindwa kufurukuta.

Bayern walionekana kukosa nguvu walizozoea na hii iliwachanganya
washabiki wa nyumbai, wakabaki na hofu hadi mechi ilipomalizika.

Kichapo dhidi ya Benfica kilikuwa cha pili tu katika mechi 21. Wana
mshambuliaji mahiri katika jina la Jonas, Mbrazili aliyefunga mabao 32
katika mashindano yote msimu huu.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version