Menu
in , ,

BAO LA BENTEKE HALIKUWA BAO HALALI

Benteke, akifunga bao, muda mfupi baada ya mwenzake kuonekana kuucheza akiwa kwenye nafasi ya "kuotea"

Liverpool jana waliwafunga AFC Bournemouth bao moja kwa sifuri na kujinyakulia alama tatu muhimu kwenye mchezo wao wa pili wa Ligi Kuu ya England msimu huu.

Bao hilo lilifungwa na Christian Benteke kwenye dakika ya 26 ya mchezo akimalizia krosi maridadi iliyopigwa na Jordan Henderson. Hata hivyo bao hili lilikuwa na utata. Utata wake unatokana na madai ya walio wengi kuwa bao hilo lilikuwa ni bao la ‘offside’.

Ingawa Benteke aliyefunga bao hilo hakuwa amezidi lakini ukilitazama bao lile na kuipitia kwa umakini sheria namba 11 ya sheria 17 za mchezo utakubaliana na mimi kuwa mwamuzi alifanya makosa kuamua kuwa lilikuwa ni bao.

Aliyezidi alikuwa ni Philipe Coutinho na kwa mujibu wa sheria hiyo namba 11 alifanya madhambi ya offside. Sheria 17 za mchezo bado hazijawahi kutafsiriwa kwa Kiswahili na mamlaka zinazohusika.

Hata hivyo hii hapa ni tafsiri rahisi lakini yenye ufanisi ya sheria namba 11 ya sheria hizo. Sheria hiyo inasema kuwa mchezaji aliyezidi atakuwa amefanya madhambi ya ‘offside’ iwapo atajihusisha moja kwa moja na mchezo kwa kufanya moja kati ya haya.

La kwanza ikiwa atauingilia mchezo kwa kuugusa ama kuucheza mpira uliopigwa ama kuguswa na mwenza wa timu yake.

La pili ni iwapo atamuingilia mpinzani kwa kumzuia asiucheze ama asiwe na uwezo wa kuucheza mpira kwa kumzibia njia ya kuuona ama kumkabili mpinzani huyo.

Na la tatu ni ikiwa mchezaji huyo ataitumia nafasi yake ya kuzidi na kumalizia mpira uliopanguliwa na golikipa ama kugonga mwamba ama vinginevyo.

Coutinho aliyekuwa amezidi hakufanya jambo la kwanza wala la tatu hapo juu. Lakini kimsingi alilifanya la pili kwa kuwa krosi ilipopigwa alijaribu kufunga lakini mpira ukampita.

Kitendo hicho kinamfanya awe amemuingilia golikipa Artur Boruc kwa kuwa alimzibia njia ya kuuona ama kuucheza na kinajitosheleza kabisa kuwa kilimuathiri golikipa huyo. Hapa ndipo Coutinho anapokuwa amefanya madhambi ya ‘offside’.

Na kwa mujibu wa sheria hiyo namba 11 mchezaji anapofanya madhabi ya offside mwamuzi anatakiwa kuitunuku timu pinzani mpira wa adhabu (free kick). Hivyo hoja ya kwamba Benteke hakuwa amezidi haina mashiko kwa kuwa tayari madhambi yalishafanywa na Philippe Coutinho.
bentekef

Baadhi ya wachambuzi wa England walisema kuwa kwa mujibu wa sheria mpya za Ligi Kuu ya England lile si bao halali kwa kuwa Coutinho alimuathiri na kumpoteza golikipa kwa kujaribu kuupiga mpira akiwa amezidi.

Kwa upande wa Gary Neville, mchezaji wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England ambaye sasa ni mchambuzi wa televisheni ya Sky Sports aliikosoa menejimenti ya EPL kwa kusema, “Wanajaribu kuishughulikia sheria ya offside kila mwaka lakini hawaiboreshi chochote”.

Hata hivyo kwa upande wangu sidhani kama kuna haja ya kuziangalia sheria ndogo ndogo za FA kwa kuwa sheria za jumla za FIFA zinatosha kabisa kuutazama uhalali wa bao alilofunga Benteke.

Kocha wa AFC Bournemouth, Eddie Howe baada ya mchezo alisema kuwa hawakuridhishwa na maamuzi ya mwamuzi Craig Pawson hivyo watakiomba chama cha waamuzi cha England kiwape maelezo juu ya bao hilo.

Hilo halitaweza kubadilisha chochote kuhusiana na matokeo ya mchezo huo. Liverpool watabaki na alama zao zote tatu walizokusanya kwenye mchezo huo.
Pia itaendelea kubakia kwenye rekodi kuwa mbaka sasa tayari Benteke
ameshaifungia Liverpool bao moja kwenye EPL. Hata hivyo bao hilo la Benteke halikuwa bao halali kwa mujibu wa sheria za FIFA.

Written by Kassim

Exit mobile version