Balotelli afungwa ‘gavana’
Mchezaji mtukutu wa Italia, Mario Balotelli aliyesajiliwa na AC Milan kwa mkopo kutoka Liverpool amewekewa kifungu kwenye mkataba wake kinachomzuia kujiingiza katika tabia mbaya.
Balotelli ambaye mwenyewe amesema kwamba sasa amekua na hatakubali kupoteza tena fursa aliyoipata kwani inaweza kummaliza kisoka, atatakiwa kuwa na nidhamu karibu kama ya mwanajeshi.
Pamoja na mambo mengine, mkataba wake unamtaka kuachana na mitindo ya hovyo ya kukata nywele, uvaaji mbaya nao ni marufuku wakati pia anatakiwa kuishi maisha kwa kuzingatia anavyotakiwa kwa ajili ya afya yake.
Gazeti la michezo la kila siku la Italia, Gazzetta dello, linaarifu kwamba vigezo vya masharti kwa Balotelli vilichukuliwa na Mtendaji Mkuu wa AC Milan, Adriano Galliani, kutoka kwenye kanuni na taratibu zinazotumiwa na watu walio katika Jeshi la Anga la Italia.
Balotelli, 25, amekuwa akichangizwa kwa tabia zake ndani na nje ya uwanja, ikiwa ni pamoja na kucheza chini ya kiwango, kujikuta matatani nyumbani kwake na mitaani, na sasa anarejea Milan kwa mkopo, mwaka mmoja tu tangu alipotoka hapo na kusajiliwa moja kwa moja na Liverpool.
Balotelli atatakiwa kuwa makini kuhakikisha hachafui picha ya klabu kwa namna yoyote, na atafuatiliwa kwa karibu katika mitandao yake ya jamii ya Twitter, Facebook na Instagram na akienda mchomo kidogo tu, hatua zitachukuliwa.
Alifuzu vipimo vyake vya afya Milan Jumanne hii hata kabla ya dili lenyewe halijakubalika wala kuthibitishwa rasmi. Ni marufuku kwa Balotelli kufanya baadhi ya mambo kupita kiasi, kama vile kwenda kwenye klabu za usiku, kuvuta sigara, kuchelewa kufika mazoezini. Unywaji wake wa kileo nao utadhibitiwa.
Akiwa Milan kipindi kilichopita hakuwa na msimu mzuri, na baada ya kucheza hovyo kwenye mojawapo ya mechi, alichagizwa na wachambuzi wa soka, na alipoulizwa maswali alikasirika kupita kiasi, akawaambia wahusika hawakuwa na uelewa wa soka, kisha akatupilia mbali kinasa sauti.
Balotelli aliadhibiwa kwa kadi baada ya kuwaonesha ishara mbaya washabiki wa Cagliari na kufungiwa kucheza mechi tatu. Alidakwa akivuta sigara kwenye maliwato iliyo kwenye treni, pale mkata na mkagua tiketi alipoingia humo baada ya kuhisi tukio kama hilo. hata hivyo, matukio hayo ni madogo ikilinganishwa na aliyofanya akiwa Manchester City, ambapo aliishia kutia moto nyumba yake baada ya kulipua fashifashi bafuni mwake.
Alimaliza vibaya kwa kukunjana na kocha na raia mwenzake wa Italia, Roberto Mancini wakati wa mazoezi baada ya kushindwa kuelewana.