Menu
in , , ,

Bado naisubiri Yanga iifikie Simba!

Bado naisubiri, sijachoka kuisubiri kwa sababu safari haiwezi kukamilika bila uwepo wake. Uwepo wa Yanga ni muhimu sana kwenye huu mpira wetu ndiyo maana bado naisubiri. Wakati nikiwa kwenye kigoda changu nikiwa naisubiri Yanga, mkononi mwangu nina magazeti mawili.

Gazeti la kwanza ni lile ambalo lilichapishwa kipindi cha harakati za uhuru wa Tanganyika. Muda umepita sana, lakini maandishi yaliyopo kwenye hili gazeti hayajapita, bado yapo na yanaishi mpaka leo.

Maandishi ya gazeti hili yamenikumbusha habari za Bibi Titi , mwanamke ambaye alikuwa bega kwa bega katika harakati za uhuru hapa nchini, ni mwanamke lakini alikuwa na ngozi ya chuma, ilihimiri mvua na jua ili uhuru wetu upatikane.

Wakati naendelea kusoma habari za Bibi Titi niligeuza gazeti langu upande wa nyuma , upande ambao mara nyingi habari za michezo huandikwa kwa wingi sana. Ndiyo upande ambao nilikutana na habari ya timu ya vijana wa Afrika , Yani Dar Youngs Afrika.

Ndiyo timu pekee ya mpira wa miguu hapa nchini iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwaunganisha vijana wa wakati huo kudai uhuru wa Tanganyika baadaye Africa.

Dar Youngs Afrika ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina maarufu kama Yanga, ilishiriki kikamilifu kwa kiasi kikubwa kwenye upatikanaji wa uhuru wa nchi baadhi za Afrika.

Unakumbuka jinsi ambavyo Dar Young Afrika ilivyompeleka aliyewahi kuwa raisi wa Msumbiji, Samora Machel baada ya kukaa muda mrefu uhamishoni akiwa Tanzania?

Dar Young Afrika ilimsindikiza mpaka Msumbiji, walipofika Msumbuji wakacheza bonge la mechi kusherehekea uhuru wa Msumbuji. Weka hiki akili mwako, Yanga ilianzwa kuundwa kwa ajili ya kupigania na kuleta uhuru, tuendelee !

Baada ya Yanga kufanikisha kumsindikiza Samora Machel, walishiriki kwenye upatikanaji wa Uhuru wa nchi kama Zimbambwe, Zambia na mpaka wakafikia hatua ya uwanja wao wa mazoezi kuuita Kaunda, ikiwa ni heshima kwa Kenneth Kaunda.

Wakati naendelea kusoma gazeti hilo la zamani, niliamua kuchukua gazeti jipya, gazeti la sasa, gazeti la kizazi kipya. Gazeti ambalo kwenye ukurasa wa michezo kuna habari kuhusu Simba SC.

Simba Sc ambao tayari wameshaanza kuingia kwenye mfumo mpya wa uendeshaji wa kisasa kwenye klabu. Simba Sc ambayo ina miliki uwanja wa kisasa wa mazoezi. Vitu ambavyo ni mabadiliko makubwa kwenye mpira wa miguu, wamechelewa lakini hatua zao zinatia matumaini.

Hatua hizi nazisubiri kwa Yanga SC, timu ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kupigania uhuru, natamani Yanga SC ipigane na ipate uhuru wa uendeshaji wa kisasa katika timu. Natamani Yanga ifike angalau sehemu ambayo Simba ipo. Bado sijachoka naendelea kuwasubiri Yanga naamini watafika muda siyo mrefu.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version