*Mchezo wa Yanga wavunjika
Azam FC wamewalaza Mwadui FC kwa mikwaju ya penati 5-3 na kukata tiketi ya kucheza fainali kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho uliopigwa ndani ya dimba la Mwadui Complex jijini Shinyanga jioni ya leo.
Mchezo huo ulihitaji dakika 30 za nyongeza kuweza kuamuliwa baada ya timu hizo kwenda sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 ambapo bao la Azam lilifungwa na Khamis Mcha ndani ya dakika ya 3 huku lile la Mwadui likifungwa ndani ya dakika ya 82.
Ni Khamis Mcha aliyewapatia Azam bao la pili akifunga ndani ya dakika ya 97 likiwa ni bao lake la pili la mchezo huo kabla ya Jabir Aziz kusawazisha kwa penati ndani ya dakika ya 120 na kufanya matokeo ya dakika 120 kuwa 2-2.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati wakaibuka washindi kwa mikwaju ya penati na kutinga fainali pale mlinzi Aggrey Morris alipotumbukiza wavuni mkwaju wa tano wa penati kwa upande wa Azam.
Nahodha John Bocco, Himid Mao, Allan Wanga na Waziri Salum pia walifunga mikwaju yao kwa upande wa Azam huku mikwaju mitatu ya Mwadui ikifungwa na Malika Ndeule, Iddi Moby na Jabir Aziz. Kevin Sabato ndiye pekee aliyekosa.
Kwingineko mchezo mwingine wa nusu fainali ya michuano hii kati ya Coastal Union na Yanga ulivunjika huko Mkwakwani jijini Tanga kutokana na vurugu za mashabiki waliokerwa na maamuzi ya utata ya mwamuzi Abdallah Kambuzi.
Mwamuzi alimaliza mchezo huo mnamo dakika ya 110 ndani dakika 30 za nyongeza Yanga wakiwa wanaongoza kwa 2-1 kutokana na washabiki wa Coastal kurusha mawe uwanjani. Taarifa zaidi juu ya hatma ya mchezo huo zinasubiriwa.
Itakumbukwa mshindi wa michuano hii atakata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika nafasi ambayo kabla ya msimu huu ilikuwa inakwenda kwa timu iliyomaliza kwenye nafasi ya pili kwenye VPL.