Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Dar-es-salaam Young Africans wamefuzu kwenda hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho baada ya jioni hii kuwalaza Ndanda FC 2-1 ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.
Mabao ya vijana hao wa Jangwani yalitumbukizwa wavuni na Paul Nonga na Kevin Yondani aliyefunga kwa mkwaju wa penati huku lile la Ndanda likiwekwa wavuni na kiungo wa zamani wa Simba Kiggi Makasi.
Ni Paul Nonga aliyewapatia Yanga bao la kuongoza mnamo dakika ya 27 ya mchezo kwa kichwa safi akiunganisha krosi ya Juma Abdul.
Bao la Nonga lilidumu mbaka kipenga kilipopulizwa na mwamuzi kuashiria kumalizika kwa dakika 45 za kwanza za mchezo.
Mnamo dakika ya 56 ya kipindi cha pili Ndanda wakasawazisha bao kupitia kwa kiungo wao Kiggi Makasi aliyemchambua vizuri Simon Msuva na kupiga shuti zuri lililozama wavuni moja kwa moja.
Dakika ya 68 ya mchezo ikamshuhudia mlinzi wa Ndanda Paul Ngalema akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi Simon Msuva kwenye eneo la hatari.
Kevin Yondani akazamisha wavuni mkwaju wa penati uliozawadiwa na mwamuzi na kufunga bao lililowakatia vijana wa Jangwani nafasi ya kucheza nusu fainali.
Kwenye mchezo mwingine mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati Azam FC wamewafunga Tanzania Prisons 3-1 ndani ya dimba la Chamazi jijini Dar-es-salaam.
Shukrani kwa Shomari Kapombe aliyeifungia Azam mabao mawili huku la tatu likifungwa na Khamis Mcha wakati Prisons wakipata bao lao kupitia kwa Jeremiah Juma.
Azam ndio waliotangulia kuziona nyavu kupitia kwa mlinzi wao wa kulia Shomari Kapombe mnamo dakika ya 9 kabla ya Jeremiah Juma kuwasawazishia Prisons kwenye dakika ya 31 ya mchezo.
Kapombe akazama tena wavuni mnamo dakika ya 60 kabla ya Khamisi Mcha kuwahakikishia Azam ushindi huo muhimu kwa kufunga bao la tatu kwenye dakika ya 86 ya mchezo.
Matokeo hayo yanawapeleka Azam na Yanga kuungana na Mwadui FC ambao walishatinga nusu fainali tangu wiki iliyopita walipowatandika Geita Gold Mine 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mchezo kati ya Simba na Coastal Union utakaopigwa tarehe 6 Aprili ndio utakaoamua timu ya nne itakayoungana na Azam, Mwadui na Yanga kwenye hatua ya nusu fainali.
Ratiba ya nusu fainali itapangwa kupitia droo itakayochezeshwa tarehe 7 Aprili na kuoneshwa moja kwa moja kwenye televisheni kuamua nani kucheza na nani kwenye hatua ya nusu fainali.
Ikumbukwe mshindi wa michuano hii ndiye atakayeiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF nafasi ambayo kabla ya msimu huu ilikuwa ikienda kwa timu iliyokamata nafasi ya pili kwenye VPL.