Ukizungumzia dhana ya michezo ni biashara na michezo ni ajira ni lazima uzungumzie suala la nguvu ya vyombo vya habari katika kurusha matangazo ya michezo (broadcasting rights). Kurushwa huko kwa michezo katika runinga ndiko kumefanya mashindano mengi ya michezo kuwa na thamani. Thamani hiyo inatokana na kwamba pindi michezo inapokuwa inarushwa mubashara imepeleka michezo mingi kuongezeka kwa mashabiki katika michezo. Mojawapo ya makampuni ambayo yamechangia kwa kiwango kikubwa ni kampuni ya ESPN ambalo lipo barani ulaya na Marekani. Kampuni hilo lilikuwa ni mojawapo ya makampuni ya mwanzo kuona fursa ya kurusha matangazo ya michezo na kuanza kutengeneza thamani ya kipesa kupitia kurushwa huko kwa matangazo. ESPN ilianzishwa mnamo mwaka 1979.
ESPN ndio walikuwa kampuni ya kwanza kutengeneza vituo vya runinga ambavyo vilikuwa vinarusha matukio ya michezo kwa masaa 24 yaani siku nzima kituo cha runinga kilikuwa kinarusha maudhui ya michezo. Kabla ya ESPN kuanza hivyo soko la vituo vya runinga vya masaa 24 havikuwepo.mmiliki wake bwana Bill Rasmussen aliona hitajio la wakazi wa mji wake wa Conecticut ambao walikuwa wanahamu sana ya kuangaliza Zaidi mechi za mchezo wa Hockey kwa hiyo akaamua kuanzisha kituo cha runinga ambacho kilirusha mechi za timu za wakazi wa mji huo na alifanikiwa kupata mtaji kwa kudunduliza kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali ambao waliwekeza kwenye kampuni yake hiyo na kisha kupewa sehemu katika umiliki wa kampuni hiyo.
Wamiliki na wafanyakazi wa ESPN walijua kwamba kuna wapenzi na mashabiki wa michezo ambao wanatamani wapate maudhui ya michezo kwenye runinga kwa masaa 24 na wakapanga mikakati na kisha kuyatekeleza ili kuhakikisha wanakata kiu ya mashabiki hao.Rasmussen na wafanyakazi wake walianza kwa kuonyesha michezo ambayo haionyeshwi na vituo vingine vya runinga
Kanuni mojawapo iliyoifanya ESPN ifanikiwe katika azma yake ya kuwa kampuni bora ya michezo ni kuwa makini sana kwenye masuala ya namna ya kuajiri watendaji wa kampuni hiyo. Jambo la kwanza kubwa ambalo kampuni hilo limekuwa linafanya ni kuhakikisha kwamba haimuajiri mfanyakazi yoyote yule mpaka ijihakikishie kwamba mtu huyo anapenda michezo kikweli toka moyoni mwake. Kupitia kanuni hiyo waliweza kupata wafanyakazi ambao walikuwa na mapenzi ya dhati na michezo na hilo liliwasaidia kuweza kuajiri watu ambao walikuwa wana uchungu na tasnia hiyo ya michezo kwani watu hao walikuwa wana mapenzi ya dhati na tasnia ya michezo kwa hiyo walikuwa wanajituma kidhati na kwa ubunifu wa hali ya juu kuhakikisha ESPN inagusa maisha ya watu kupitia michezo.
Kwa sasa kampuni hiyo imetanuka sana na kufikia hatua ya kuanzisha makampuni tanzu ambayo yako chini ya kampuni mama. Makampuni hayo ni kama ifuatavyo: ESPN2, ESPN NEWS, ESPNU, ESPN Deportes, and ESPN Classic. Piling on, ESPN the Magazine, ESPN the store, ESPN Radio, ESPN Zone Restaurants, ESPN.com, ESPN Books, ESPN Original Entertainment (Movies and Shows), the X Games, ESPY. Kwa sasa kampuni hiyo imekuwa kampuni kubwa sana na ina waajiriwa wengi sana na imegusa maisha ya watu wengi sana. Thamani ya ESPN kwa sasa ni dola za kimarekani bilioni 28.
Azam media ni kampuni ambayo inakuwa kwa kasi sana katika ukanda wa afrika mashariki na kati. Ina miaka 10 tu toka ianzishwe na inajivunia kukuza michezo katika ukanda huo. Kabla ya uwepo wa Azam media mechi za soka hazikuwa zinaonyeshwa mubashara (live). Kituo hicho kimechangia kukua kwa michezo kadhaa nchini Tanzania na nchi za jirani. Kampuni hiyo imekuwa kwa miaka kadhaa inarusha matangazo ya moja kwa moja ya ligi kuu ya soka nchini Tanzania bara, Kenya, Uganda na Rwanda. Halikadhalika kampuni hiyo imesaidia sana kukua kwa mchezo wa ngumi kwa kuyarusha mubashara mapambano ya ngumi (boxing) katika maeneo kadhaa ukanda wa afrika mashariki na kati. Halikadhalika wamekuwa wanajaribu kuyakuza michezo midogo kama vile riadha, mashindano ya magari na kadhalika.
Katika mchezo wa soka Azam media wameenda mbali Zaidi na kutoa udhamini wa fedha kwa vilabu ambavyo vinashiriki ligi kuu ili kutoa motisha. Udhamini huo umesababisha ushindani katika ligi kuu ya soka Tanzania umekuwa sana na umechangia hata kwa timu ya taifa kuwa ni yenye ushindani na hatimaye kufanikiwa kufuzu kushiriki AFCON kwa mara 2 huku vikosi ambavyo vimeshiriki vikiwa vimesheheni wachezaji wengi ambao wanaocheza ligi ya ndani. Udhamini huo umesaidia kuongeza wigo wa ajira kwa wadau wa soka na michezo kupitia kuonyeshwa mubashara kwa mechi za mashindano.
Udhamini wa Azam umepeleka michezo kukua nchini Zaidi na kuzidi kuwa ni biashara kwani kwa sasa wawekezaji wameongezeka katika ligi kwani tumeona hata Startimes wameanza kujitanua na kuanza kudhamini michezo nchini Tanzania kwa kudhamini matukio kadhaa ya michezo nchini. Hakika kampuni ya Azam inatakiwa ipewe maua yake kutokana na mchango wake mkubwa katika tasnia ya michezo nchini.