Timu ya Azam imeweka historia kwa kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa soka Tanzania.
Azam ambao hadi sasa hawajafungwa mechi yoyote walifanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuwanyoa Mbeya City wana Amsha Amsha kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 inajulikana kwa mipango yake mizuri ndani na nje ya uwanja, ambapo inaelezwa uwa na wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi.
Azam wametawazwa kuwa mabingwa baada ya kuwatoa Mbeya City jasho kwa mabao 2-1, yake yakifungwa na Gaudance Mwaikimba na John Bocco wakati Mwigane Yeya alifunga la upande wa Mbeya.
Azam wamefikisha pointi 59 ambazo haziwezi tena kufikiwa na wapinzani wao wa karibu, Yanga ambaow amefikisha pointi 55. Wakishinda mechi dhidi ya Simba watafikisha pointi 58 na hata kama Azam watafungwa kwenye mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu watabaki ndio wafalme wa soka. Mbeya City wamebaki nafasi ya tatu.
Azam wataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika msimu ujao wakati Yanga watacheza Kombe la Shirikisho, klabu hizo mbili zikiwa zimebadilishana kwani msimu huu Yanga ndio walishiriki Klabu Bingwa Afrika.
Yanga watajilaumu wenyewe kwa kushindwa mara kadhaa kufukia pointi za Azam, kwani walipocheza dhidi yao walikuwa mbele kwa bao moja, wakapata penati wakakosa, mchezaji wa Azam akatolewa hivyo wakacheza dhidi ya wachezaji 10 kisha bao likasawazishwa.
Kadhalika walipokwenda Tanga majuzi walichapwa na timu ndogo ya Mgambo na sasa itabidi wajipange kwa ajili ya msimu ujao